BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesema watalii 700 kutoka nchini Israel watawasili nchini mwezi huu na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.
Kati ya watalii hao, zaidi ya 150 wanatarajiwa kufika nchini kuanzia kesho na watatua katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na kisha kwenda kwenye vivutio vya utalii.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema watalii hao watakuwepo nchini kwa wiki nzima na watondoka Agosti 9 kurudi nchini kwao.
“Wakati hawa wakiondoka Agosti 9, siku hiyo hiyo ndege nyingine itatua ikiwa na watalii 200 kutoka Israel. Hawa watakaa hapa nchini mpaka Agosti 16 na Agosti 10 itakuja ndege nyingine ya watalii zaidi ya 150 ambayo itatua moja kwa moja Zanzibar na wataondoka Agosti 18,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Mihayo, Agosti 17 ndege nyingine ikiwa na watalii zaidi ya 200 itakuja nchini na kutua KIA ambao watakaa mpaka Agosti 24, mwaka huu. Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa watalii kutoka Israel kuja nchini na tangu Aprili hadi Mei walikuwa wakituma watu wao kuja kuangalia hali ilivyo nchini.
“Kuna wakati walikuja madaktari tisa kutoka Israel na kwenda kwenye hifadhi za Tanzania kuangalia hali ya usalama,” alisema.
Aidha, alisema atakutana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ili aweke kipaumbele kwa waongoza watalii kupatiwa chanjo kwa lengo la kuwaongezea imani watalii kuwa Tanzania ni salama.
Aprili 20, mwaka 2019, watalii 1,000 kutoka Israel waliwasili nchini katika ndege nne kubwa katika kiwanja cha KIA na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.