Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesitisha watalii 10,000 kutoka China kuingia Tanzania kwa ajili ya kudhibiti maambuzi ya virusi vya corona yaliyoikumba nchi hiyo ya bara la Asia.
Watalii hao walikuwa wanaletwa Tanzania na kampuni ya Touchroad International Holdings Group.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Januari 27, 2020 na mwenyekiti wa bodi hiyo, Jaji Thomas Mihayo inaeleza kuwa wamesitisha ujio wa watalii hao baada ya Serikali ya China kuzuia wananchi wake kusafiri nje ya nchi hiyo kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Jaji Mihayo amesema Desemba 2019 bodi hiyo na kampuni ya Touchroad waliisaini makubaliano ya ushirikiano wa kuleta watalii 10, 000 kutoka China.
"Napenda kuchukua fursa hii kwa masikitiko kuwajulisha safari hizo za ndege maalumu za ATCL kuleta watalii zilizopangwa kufanyika Februari 24 na Machi 2, 2020 zimeahirishwa baada ya serikali ya China kuzuia wananchi wake kusafiri nje ya nchi hiyo,” anaeleza Jaji Mihayo katika taarifa hiyo.
Amesema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kampuni hiyo, ujio wa watalii hao umezuiwa kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.