Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watalaamu wasaka suluhu vifungashio bora

4bd08bb7d86c00085f9508ae5098a8c4 Watalaamu wasaka suluhu vifungashio bora

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWEZI uliopita, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitoa hadi Desemba 31, mwaka huu kuwa ni siku ya mwisho ya utumiaji wa vifungashio vya chupa za maji, karanga au ubuyu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka, hivi karibuni limekuwapo ongezeko la uzalishaji wa vifungashio vya plastiki ambavyo chanzo chake hakijulikani na ni vifungashio ambavyo havina kibali cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Dk Gwamaka amesema utengenezaji, usambazaji na matumizi ya vitu hivyo ni uvunjaji wa Kanuni Na 3 na 4 za Sheria ya Mazingira ya 2004, ambazo zilitungwa na kutangazwa 2019 ili kutekeleza katazo la serikali la matumizi ya plastiki.

“Kanuni namba 3 inawataka wazalishaji kuwa na kibali kutoka TBS baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, lakini hali haiko hivyo kwa sasa,” anasema Dk Gwamaka.

Aliongeza kuwa kuwapo kwa vifungashio hivyo sokoni ni kinyume cha Kanuni ya 4 (b) na (c) ambayo imetungwa na kutangazwa ili kulinda afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa kanuni za upigaji marufuku mifuko ya plastiki, ni marufuku kutengeneza, kuuza, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, baraza lazima lisimamie sheria na kuzuia matumizi ya bidhaa zisizoruhusiwa kisheria, alisema Dk Gwamaka. Baraza limetaka watumie vifungashio mbadala vilivyoelekezwa kutumika kwa ajili ya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Gwamaka, hakutakuwa na huruma kwa mfanyabiashara yeyote atakayekaidi agizo hilo kwani serikali imeamua kuzitafsiri kwa vitendo kanuni na sheria, zinazoongoza katazo hilo linalolenga kulinda mazingira.

“Wingi wa aina hiyo ya mifuko unaondoa mantiki na lengo nzima la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki pia kuongezeka kwa mifuko hiyo na jinsi ilivyobadilishwa matumizi na wananchi,” alionya Dk Gwamaka.

Aliongeza kuwa mifuko aina hiyo inachangia kuua viwanda vya ndani na serikali kukosa kodi stahiki.

“Kuna wafanyabiashara wameendelea kuzalisha vifungashio vya plastiki ambavyo vilipigwa marufuku tangu Juni Mosi 2019. Kuendelea kuzalisha mifuko hiyo ni kukiuka kanuni, taratibu na sheria za mazingira zinazoongoza katazo la matumizi ya mifuko hiyo,” alifafanua.

Akifafanua, alisema vifungashio hivyo vya plastiki aina ya ‘tubing’ ambavyo vinatumika kufungia vitu kama karanga, ubuyu na barafu, sasa vinazalishwa kwa wingi na ukubwa tofauti na kutumika kama vibebeo kwa bidhaa za sokoni.

Alisema kubaki kwa vifungashio vya ‘tubing’ ilikuwa ni kwa hisani ya serikali na siyo takwa la kisheria au kanuni, zinazopiga marufuku matumizi ya plastiki. Lakini, kutokana na wingi wake mitaani, hakuna sababu ya kuendelea kubaki na huruma hiyo, kwa maana kuwa madhara yake hayatofautiani na mifuko mingine yoyote ya plastiki.

Aliongeza kuwa marufuku ya ‘tubing, itasaidia kuwabana wazalishaji wasio rasmi, kulinda afya za watu na mazingira, kutengeneza ajira, kurahisisha ufuatiliaji wa sheria na kulinda wafanyabiashara waaminifu.

Kutokana na hatua hiyo, viongozi wa NEMC, TBS, watengenezaji, wasambazaji na wasafirishaji wa vifungashio vya plastiki wamekutana hivi karibuni na pande zote zimekubaliana maridhiano na kuelimishana kabla ya kutumia sheria ni kati ya mambo muhimu katika kupalilia utulivu wa kijamii nchini.

Kutokana na mkutano ulioitishwa na NEMC, sasa kuna matumaini kwamba upo uwezekano wa kupata vifungashio vyenye viwango vinavyokubaliwa na roho za wafanyabiashara wadogo zinaanza kutulia.

Mamilioni ya Watanzania wanajiajiri katika sekta ya uchumi isiyo rasmi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Abdallah Mwinyi alieleza vizuri umuhimu wa wafanyabiashara wadogo wakati wa mkutano, akisema wafanyabiashara wadogo ndiyo watoaji wa huduma kwa watumiaji wa mwisho.

Biashara wazifanyazo wajasiriamali ndiyo msingi wa riziki zao na biashara hizo ndizo zinazowapa uwezo wa kutatua matatizo ya kijamii kama kusomesha watoto, kushiriki katika misiba na harusi na kulipa kodi.

Nayo kauli ya Mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Sufiani, ni uthibitisho kwamba ukiwepo ushirikishwaji, mashauriano na maridhiano jambo gumu la kutisha linakuwa jepesi.

NEMC iliandaa mkutano huo ili wadau wajadilili tatizo la kitaifa la kuondoa vifungashio vya plastiki. Mkutano huo umekuwa ni ushahidi kwamba yameanza kuwepo mawazo mapya katika utumishi wa serikali; mawazo ya kuwasikiliza wadau badala ya kuwaburuza au kutumia tu sheria na vitisho.

“Tunawashukuru NEMC kutukutunisha hapa na kufafanua vizuri juu ya sheria na kanuni zinazopelekea kuwepo kwa katazo. Tumepata ufafanuzi lakini tunaomba tupate muda wa kukutana zaidi kwa majadiliano,” alisema Sufiani na kuongeza kwamba wazalishaji na wawekezaji ni Watanzania wazalendo kama watu wengine.

“Hatukusudii kukaidi sheria. Tulio wengi tumeelewa tunachotakiwa kufanya. Kutekeleza sheria hiyo kuna mambo mengi ya kitaalamu ambayo hayawezi kukamilika kwa muda mfupi ambao umetolewa.

“Hatupendi kuwa sehemu ya watu wanaokaidi sheria na ndiyo maana tumekuja kuwasikiliza na bahati nzuri wametueleza mambo mazuri. Tutarudi na kuongea na watalaamu wetu ili kubadilisha dizaini za mashine lakini pia kuona ni kwa namna gani baraza linatekeleza sheria hiyo pasipo kuathiri biashara,” aliongeza mwakilishi huyo wa CTI.

Baada ya uchangiaji huru wa maoni, Mkurugenzi wa Upimaji na Ugezi wa TBS, Johanes Maganga aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wake aliwahakikishia wadau kuwa TBS itatoa ushirikiano na kupokea maoni na ushauri wa wadau.

“TBS inasimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa kwa mujibu wa sheria na tutashirikiana na wawekezaji ili waweze kupata “certification” ya bidhaa zao kabla ya Desemba 31,” alieleza Maganga.

Alifafanua kuwa mbali ya TBS kusimamia sheria, shirika linashauri pia juu ya upungufu ambao unatokana na uzalishaji wa bidhaa. “Tutafanya kazi kwa ukaribu na wadau wote hususani wenye viwanda ambavyo wanazalisha vifungashio na kuwapa vibali iwapo watakidhi vigezo tunavyoviweka,” alisema.

Maganga ameeleza kuwa TBS haikusudii kukwamisha azma ya serikali ya ujenzi wa viwanda ifikapo 2025 na hivyo itafanya kila kitu kuhakikisha wawekezaji wanaendelea kufurahia kuwekeza nchini.

“Mkutano ulilenga kuwanufaisha wawekezaji ambao wamekuwa wakitoa kodi kubwa kupitia uzalishaji wanaofanya. TBS tunaendelea kusisitiza ubora wa bidhaa ili kuleta ushindani wa kweli na sio kuwabeba wachache ambao wamekuwa na bidhaa zisizo na viwango na hatujui hata bidhaa hizo zinapozalishwa,” alieleza.

Amewahakikishia wawekezaji kuwa TBS pia inatoa ushauri juu ya upungufu katika utengenezaji wa bidhaa na kuwataka wawekezaji kuacha kuzifikiria taasisi kama vyombo vya kudai tozo na kutoa faini tu.

“Wito wangu kwa wawekezaji ni kwamba msizitame taasisi kama NEMC, TBS na zingine zinazohusika na mambo ya uwekezaji kama taasisi ambazo zinadai tozo tu kwa kila kosa linalopatikana. Tunayo nafasi ya kushauri pia ili kuleta ufanisi zaidi,” alieleza.

Aidha, Mwinyi amependekeza kuwa wakati sheria na kanuni zinapotungwa ni vyema kuwahusisha wafanyabiashara wadogo kwa sababu ya umuhimu wao.

“NEMC na TBS wameeleza mambo mengi kisheria na kanuni zinazohusu mazingira ambazo tulio wengi hatukuzifahamu hapo awali, imetupa mwanga juu ya nini cha kufanya, lakini ningependekeza kwamba sheria hizi zinapotungwa ni vyema zikawa zinawahusisha wadau wote ili zisiwe zinaleta maumivu,” alisema.

NEMC imeandaa mkutano huo siku chache baada ya kutoa tamko kwamba utumiaji wa vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango vya TBS mwisho wake ni Desemba 31, mwaka huu ili kuyanusuru mazingira.

Tamko hilo la NEMC ni mwendelezo wa hatua za kunusuru mazingira baada ya kuondoa matumizi ya mifuko ya plastiki sokoni tangu Juni 30, 2019. Mifuko ya plastiki iliondolewa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa katazo la serikali ndani ya Bunge na NEMC ikapewa jukumu la kusimamia katazo hilo.

Chanzo: habarileo.co.tz