Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kushawishi kuundwa vyama vya wafugaji

7c297cf470599c5ce7d7709c89884310 Watakiwa kushawishi kuundwa vyama vya wafugaji

Sun, 14 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAOFISA ufugaji na uvuvi wametakiwa kuunda vyama vya wafugaji katika ngazi za wilaya na vijiji zitakazosaidia kupata kero za wafugaji kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuunda kamati za majosho ya kuogeshea mifugo.

Aliyasema hayo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul kwenye mafunzo ya maofisa ugani mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara yaliyolenga kuwajengea uwezo.

Alieleza kuwa maofisa mifugo wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatafuta wafugaji na kufanya nao vikao mbalimbali vya kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma za mifugo ili sekta hiyo iweze kwenda na wakati.

Gekuli alisema anatarajia baada ya miezi mitatu kusikia mikoa ya kanda ya kaskazini wana vyama vya wafugaji mpaka kwenye ngazi za vijiji na inawezekana kwani madiwani kwa kushirikiana na maofisa ufugaji wanauwezo mkubwa wa kuwafikia wafugaji hao

Alisema ni vyema maofisa hao kuhakikikisha wanafufua majosho ambayo yapo katika maeneo yao na kuwapa chanjo mifugo ikiwa ni pamoja na kuwashauri wafugaji kulisha mifugo malisho mazuri ili waweze kuachana na ng'ombe waliokomaa misuli ambao mara nyingi nyama yao inakuwa ni ngumu.

Gekuli alisema anatamani mifugo ichakatwe ndani ya nchi ili iwe inaongeza pato la nchi badala ya kusafirisha ng'ombe kwenda kuchakatwa nchi za jirani ambapo ng'ombe mmoja hugharimu elfu 25 kusafirishwa mpaka nchi jirani ya Kenya ambapo akishachakatwa huko tozo zote zinaenda kwenye serikari ya Kenya jambo aliloeleza ni kuinyima serikali ya Tanzania mapato.

Mkurugenzi wa mafunzo, utafiti na ugani kutoka wizara ya mifugo na kilimo Dk Angelo Mwilawa alisema lengo la kuwakutanisha wataalamu hao ni kuwajengea uwezo na maarifa mapya katika utoaji wa huduma kwani wizara ya mifugo na uvuvi wamekuwa wakishirikiana na ofisi ya Rais Tamisemi kuhakikisha maafisa ugani walionao wanajengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao .

"Wizara imekuwa katika juhudi za kuhakikisha tunaweza kudhibiti magonjwa ya mifugo mbalimbali katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo sahihi na kufuata kalenda za chanjo,” alisema Mwilawa.

Alisema wizara pia inahimiza matumizi ya dawa sahihi kwani kumekuwa na watoaji wa huduma watu mbalimbali ambao wengine hawana ujuzi au utaalamu wa kazi hizo hivyo wizara kupitia baraza lao la vetenari wamekuwa wakisisitiza wataalamu walioidhinishwa na baraza ndio watoa huduma hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz