Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watakiwa kuchangamkia sumu ya nyuki

B96181448a91822591e117b17b8e238b Nyuki

Tue, 5 Jul 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wakulima wametakiwa kuchangamkia fursa ya zao jipya la sumu ya nyuki, ambayo inatumika kutengeneza dawa mbalimbali zikiwemo za mfumo wa hisia (nerves), maumivu makali ya viungo pamoja na kuchanganya kwenye vipodozi.

Mbunifu wa mashine zinazotumika kuvuna sumu ya nyuki ambaye yupo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Patrick Kitosi,amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.

Kitosi amesema mbali na kutibu magonjwa hayo, hivi sasa sumu hiyo inafanyiwa utafiti juu ya uwezekano wa kutengeneza dawa ya kansa na kuongeza kinga mwilini kwa magonjwa kama ukimwi.

Amesema kwa kushirikiana na tume hiyo, wametengeneza mashine za kisasa kwa ajili ya kusaidia wafugaji wa nyuki nchini kuvuna sumu hiyo ambayo ikivunwa inauzwa kwa kuwa ina matumizi mbalimbali kwenye sekta ya afya.

Amesema utafiti huo ulianza mwaka 2017 na hivi sasa sumu hiyo ipo kwenye hatua ya bidhaa ambayo imeanza kuuzwa kwa wakulima.

“Mashine moja inakusanya sumu kuanzia gramu 0.6 mpaka 1.5 ndani ya nusu saa. Gramu moja ya sumu hiyo inauzwa kuanzia sh 50,000 hadi Sh 350,000 soko la nje kulingana na ubora wake kwani gharama inategemea viwango,” amesema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz