Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataka Udart ipate mshindani

Kimara Mwendokasiii Mwendokasiiiii Wataka Udart ipate mshindani

Fri, 13 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati kukiwa na adha ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka, wananchi wanaotumia usafiri huo wameshauri kutafutwe mshindani ili kuboresha huduma hiyo.

Mabasi hayo, maarufu kama mwendokasi, yanasimamiwa na Kampuni ya Usafirishaji wa Mabasi yaendayo Haraka (Udart).

Maoni hayo yalitolewa jijini hapa jana kwa nyakati tofauti na wananchi, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kufika Kituo cha Mbezi, kujionea hali ya utoaji wa huduma ya usafiri huo inavyoendelea.

Hata hivyo, kupitia katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi, wananchi pia waliandika maoni yao wakiitaka Serikali itafute mtoa huduma mwingine atakayeleta ushindani sokoni badala ya kumtegemea aliyekuwepo peke yake.

Akizungumza mbele ya Chalamila, mfanyabiashara wa Stendi ya Mbezi, Joram John amesema usafiri huo wanaupenda lakini una changamoto nyingi.

“Mkuu huu usafiri ni mzuri sana, wananchi tunaupenda kwa kuwa unaturahisishia kusafiri, lakini hebu fanyeni mabadiliko kwa kuongeza wabia wengine wa kuuendesha badala ya kumwachia mmoja,” amesema John.

Maoni ya John yaliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa, Chalamila akisema, “tunahitaji maoni ya watu wenye akili kama ninyi, Dart mmesikia haya maoni, muende mkayafanyie kazi kwa sababu lengo letu sote ni kuboresha usafiri huu. Hata mimi natamani kuwe na mtoa huduma zaidi ya mmoja.”

Amesema wakati ujenzi wa barabara za kupita mabasi hayo ukiongezeka, angetamani kuona kila ruti inakuwa na mwendeshaji mwingine, hali itakayosaidia kuleta ushindani na wananchi kupata huduma bora.

Walichosema wadau Wadau wa usafirishaji, akiwamo Mataka Abdallah, walisema shida kubwa ni ubovu wa magari yanayotumiwa katika usafiri huo.

Abdallah, ambaye ni mmiliki wa daladala amesema mazingira ya Dar es Salaam ni ya joto yanayohitaji magari aina kama ya Scania kufanya kazi hiyo na si yanayotumiwa na Udart hivi sasa.

Amesema awali wakati wanashirikishwa kutoa mawazo kuhusu mradi huo, walipendekeza aina ya mabasi yanayofaa kutumika, lakini mawazo yao hayakufanyiwa kazi.

“Na sasa matokeo yake wanayaona, kila siku yanaharibika,” alisema Abdallah, ambaye alishawahi kuwa Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Wilaya ya Ilala (Wazawa).

Akizungumzia uwekezaji, mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Break Salim Break, amesema kama wamiliki wa daladala wapo tayari kuwa wawekezaji katika mradi huo, wapatiwe njia moja hata kwa majaribio.

“Humu kwenye biashara ya daladala wapo watu wanamiliki daladala hadi 70, sembuse hizo gari, watupe hata njia moja waone kama hatutaweza, tunachohitaji ni dhamana tu ya Serikali,” alisema Break.

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema kama itawezekana, Serikali ijitoe katika biashara hiyo iendelee na kazi ya kujenga miundombinu pekee.

“Lakini jingine iruhusu kuwepo kwa wawekezaji zaidi ya watatu katika njia moja kusudi msafiri aamue anapanda basi gani, yaani iwe kama ilivyo mabasi ya mikoani au daladala,” ameshauri Profesa Kinyondo.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude amesema haoni tatizo kama Serikali itaamua kuongeza wawekezaji wala mabasi, bali anachokiona ni waliopewa idhini ya kuendesha mradi huo kushindwa kujipanga vizuri na magari waliyonayo.

Mkude amesema kupitia idadi hiyo ndogo ya mabasi, mwekezaji angeweza kuweka mabasi mengine yakaanzia safari vituo vya katikati ili kuepusha wengine wasubiri katika vituo hivyo muda mrefu au kupanda gari likiwa tayari limejaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live