Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga ametoa wito kwa watafiti, wataalamu na wanasayansi ya bahari kujadili kwa pamoja namna bora ya kutunza, kusimamia na kuwekeza katika rasilimali za bahari zilizopo nchini ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Bi. Maganga ametoa wito huo hii leo Machi 27, 2023, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Warsha ya Uhakiki wa Taarifa ya Upembuzi yakinifu wa awali kuhusu Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Bahari (MSP) kwa Nchi za Magharibi mwa Bahari ya Hindi iliyoandaliwa na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amesema kuwepo kwa mpango shirikishi wa matumizi ya maeneo ya bahari ni sehemu ya suluhisho la kuleta matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa kuzingatia utunzaji sahihi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Kuna fursa nyingi katika matumizi ya Bahari ambazo zikifanyika kwa namna endelevu zitachangia katika ukuaji wa Uchumi. Shughuli kama vile uvuvi mdogo, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji samaki na mazao ya baharini zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Buluu na hatimaye kukuza uchumi wa nchi” amesema Bi. Maganga.
Aidha, ameeleza kuwa Malengo ya Umoja wa Mataifa hasa lengo Namba 14 la Maendeleo Endelevu linasisitiza matumizi endelevu ya bahari, ambapo lengo hilo linakwenda sambamba na malengo ya warsha hiyo inayohimiza kupitia na kuhakiki taarifa ya upembuzi yakinifu wa awali wa Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Bahari.
Hata hivyo ameongeza kuwa mpango huo umekuja katika wakati mwafaka ambapo Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar zikiwa zimejipanga katika kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili ujenga uchumi imara.