Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watafiti UDSM waleta kicheko kwa wafugaji samaki

Samaki Pic Watafiti UDSM waleta kicheko kwa wafugaji samaki

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimevumbua teknolojia ya kuwafanya samaki wasiwe na jinsi, lengo likiwa ni kupunguza gharama za ufugaji.

Aidha, chuo hicho kimevumbua malighafi mbadala ya utengazaji wa chakula cha samaki ambapo badala ya kutumia kundekunde na dagaa, wanatumia unga wa mmea unaojulikana kama ‘phytoplankton’.

Phytoplankton ni mimea midogo sana inayozunguka katika maji na huzalisha oksijeni na chakula kwa viumbe vya baharini.

Akizungumza na Mwananchi, katika viwanja vya maonyesho ya Nanenane jijini Dodoma, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Ndaki ya Sayansi za Maji na Teknolojia za Uvuvi, Jostus Mwijage alisema kuna aina mbili ambazo wanaweza kubadilisha jinsi hizo ikiwa ni ya homoni na ‘shocking’ (kuongeza joto).

Alisema wanapoandaa vifaranga wa samaki wa kiume(yy), wanachofanya ni kuingia katika bwawa na kuwanyang’anya wale samaki wa kike mayai kutoka mdomoni mwao ambayo yamesha yamerutubishwa na wale wa kiume.

Alisema katika mfumo wa kuangulia vifaranga hao, wana maji yanayotembea muda wote ambayo kazi yake ni kusaidia katika utotoaji kwa sababu mayai yanapokuwa kwenye mdomo wa samaki huwa anaingiza na kutoa maji.

“Hii inasababisha mayai yabaki katika movement (mzunguko) kwa maana yakitulia yatashambuliwa na vimelea na mwishowe yataoza ama yataharibika rangi kabisa na yasifae katika kutumika tena,”alisema.

Alisema shughuli ya utotoaji huo huchukua huchukua muda wa siku saba hadi 14 ambapo vifaranga vidogo mithili ya viluilui vya chura hutokea.

Alisema baada ya kutotolewa kwa vifaranga hivyo, kuviweka katika chombo kidogo ama tanki dogo na kuanza kuhudumia kwa kuwapa chakula ambacho kimechanganywa na homoni.

Alisema mfumo mwingine ni shocking (kushtua) ambapo mayai ya samaki yaliyorutubishwa yanashtuliwa kwa kuongeza joto na hivyo kusababisha kiini cha yai kisigawanyike na kuweza kutengeneza samaki wa kike.

“Samaki wasioweza kuzaliana wana faida nyingi ikiwemo kuvumilia magonjwa na pia wanakua kwa haraka kwa kuwa nguvu nyingi wanaitumia katika ukuaji badala ya kuzaa,”alisema.

Mwijage alisema lengo la kufanya utafiti huo ni kupata samaki wanaokua kwa kasi na kwa muda mfupi, ili kumpunguzia gharama mfugaji zinazotokana na kutumia muda mrefu kukuza samaki.

Pia alisema kwa kutumia teknolojia hiyo, kunasaidia mfugaji kuwa na aina moja ya uzito wa samaki walio katika bwawa lake kwa sababu hakuna wanaozaliana kipindi cha ufugaji. Alisema vifaranga hao hupatikana katika kampuni ya Big Fish Farm iliyoko Kigamboni jijini Dar es Salaam na UDSM lakini wanawashauri watakaowataka kwenda katika kampuni hiyo.

Mbadala wa dagaa na kunde

Mwijage alisema virutubisho vilivyokuwa vikitumika kutengenezea vyakula vya samaki sasa hivi vinatumika kutengenezea vyakula vya mifugo mingine, jambo ambalo linasababisha ushindani kwa kuwa mahitaji ni makubwa.

Alisema ushindani huo umesababisha bei ya vyakula kuwa juu lakini kupitia utafiti waliofanya wamegundua phytoplankton ambayo ina asilimia 56 ya protini inayotakiwa kwa samaki na inaweza kutumika kama mbadala wa dagaa na kunde.

Hata hivyo, Mwijage alisema utafiti uliofanyika barani Asia ulibaini kuwa zipo aina 60 za mmea aina ya phytoplankton, ambazo baadhi ni sumu kwa samaki.

Alisema mfugaji anapaswa kupata mtaalamu atakayeangalia ni aina gani ya mmea ambao una faida katika bwawa la samaki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live