Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu masoko ya mitaji wawa lulu

8845 Pic+wataalam TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati waombaji waliojitokeza kushiriki mafunzo ya utendaji yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana ya Uingereza (CISI) wakizidi malengo, wadau wameshauri kila wilaya iwe na mtaalamu wa masoko ya mitaji.

Mafunzo hayo ya watendaji wa masoko ya mitaji yaliandaliwa kwa ajili ya watu 40, lakini waliojitokeza kuomba kushiriki ni 64 ambao wote walipewa nafasi hiyo ili kuongeza wataalamu hao nchini.

Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji kuwezesha masoko ya mitaji kuwa na watendaji wenye weledi wa kukuza uwekezaji kupitia masoko hayo.

“Mwitikio huu unatokana na ongezeko la uelewa na uhitaji wa wataalamu wa masuala ya masoko ya mitaji nchini,” alisema Mkama.

Naye ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Orbit Securities, Simon Juventus alisema wataalamu hao ni muhimu ili kuongeza ushiriki wa wananchi na kampuni za ndani kwenye masoko ya mitaji.

“Tunazo kampuni nyingi nchini lakini ni chache zimeorodheshwa soko la hisa. Watu wanawekeza bila mpangilio kwa kukosa ushauri wa kitaalamu. Pia, wataalamu hawa wanahitajika mikoani, ikiwezekana kila wilaya iwe nayo kama ilivyo kwa wanasheria au wahasibu,” alisema Juventus.

Alifafanua kuwa wataalamu hao watasaidia kutoa elimu itakayoongeza ushawishi wa wengi kushiriki soko la hisa. Vilevile, alikumbusha kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa bado idadi ya wataalamu waliopo ni wachache.

“Tangu soko lianze ni kama miaka 20 hivi. Angalia kwa upande wa CPA iliyoanza kutolewa miaka mingi nyuma lakini mpaka leo wahasibu hawatoshi,” alisema.

Sheria inamtaka mtu yeyote anayetaka kutoa huduma katika masoko ya mitaji kama dalali wa soko la hisa au mwakilishi wake, mshauri wa uwekezaji au mwakilishi wake, mshauri mteule au mwakilishi wake au mtendaji yeyote lazima apitie mafunzo yanayotolewa na mamlaka hiyo na kufaulu mtihani unaotolewa mwishoni mwa mafunzo.

Chanzo: mwananchi.co.tz