Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wataalamu madini Tanzania, Burundi wajadili ushirikiano

64816515107fc066324f6c37b0872e3f Wataalamu madini Tanzania, Burundi wajadili ushirikiano

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATAALAMU wa madini kutoka Tanzania na Burundi wamekutana mjini Kigoma kujadili namna ya kukuza ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya madini baina ya nchi hizo.

Mkutano huo wa wataalamu wa madini unakuja kutokana na ziara ya Rais wa Burundi, Everist Ndayishimye aliyoifanya nchini Tanzania na kuwa na kikao na Rais John Magufuli walipokubaliana kukuza ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya madini baina ya nchi hizi.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa majadiliano, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk Jilly Maleko, alisema mkutano huo unatangulia kufuatia kuwepo kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi (JPC) unaotarajia kufanyika mwezi ujao.

Balozi Maleko alisema zipo fursa kubwa za kibiashara na ushirikiano katika sekta ya madini kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi hizo, hivyo majadiliano hayo na kufanyika kwa mkutano huo kutawezesha sekta ya madini katika nchi hizo kupiga hatua kimaendeleo.

Naye Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Kabura Cyriaque, alisema vikao vya ujirani mwema vimekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na biashara na kwamba, sekta ya madini itakuwa ni sehemu ya majadiliano kwenye vikao hivyo vya ujirani mwema.

Cyriaque alisema upo mradi wa barabara na reli kutoka Tanzania hadi Msongati nchini Burundi kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo DRC) ukilenga kwenda kwenye machimbo ya madini ya nikel na kwamba, majadiliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye, alisema mkoa huo una aina mbalimbali za madini ambayo ni fursa kubwa za kiuchumi na kibiashara baina ya Tanzania na Burundi.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma, Samwel Tenga, Andengenye alisema Mkoa wa Kigoma una madini mbalimbali ambayo ni fursa hata kwa wawekezaji kutoka nje kuwekeza yakiwamo madini ya viwandani, ujenzi, madini ya metal na madini ya vito ambayo mengine kwa sasa hayajawahi kuchimbwa.

Chanzo: habarileo.co.tz