Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washiriki maonesho EAC waomba vikwazo viondolewe

Maonesho EAC.jpeg Washiriki maonesho EAC waomba vikwazo viondolewe

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Washiriki wa Maonesho ya Kibiashara Afrika Mashariki yanayofanyika mkoani Kagera, wameziomba serikali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuungana na kuondoa vikwazo vilivyopo mipakani dhidi ya wafanyabiashara wanaposhiriki maonesho.

Walibainisha hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Charles Mbuge katika ufunguzi wa maonesho hayo uliofanyika mwanzoni mwa wiki. Katika maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo ‘Biashara, Viwanda na Utalii ni Nguvu Kubwa ya Uchumi, Tuichangamkie’, wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 200 wenye bidhaa mbalimbali wamejitokeza.

Wafanyabiashara hao ni kutoka Rwanda, Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na mwenyeji Tanzania. Kutokana na maombi hayo, Nguvila alitoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji kupitia upya vikwazo vilivyopo mpakani ili kuwezesha wafanyabiashara kuwa huru na kushiriki maonesho nchini bila vikwazo.

Wafanyabiashara hao kutoka nchi mbalimbali za EAC walilalamikia bidhaa zao kukwama mpakani na kuwekewa vikwazo huku baadhi wakilipishwa tozo nyingi. Mshiriki kutoka Uganda, Josephine Josephat, alisema ingawa mambo mengi yamerekebishwa na vikwazo vingi kuondolewa, bado kuna changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi ili kukuza maonesho hayo na kuyafanya yaongeze tija.

Kwa mujibu wa Josephine, vikwazo vinavyowakumba mipakani ni pamoja na mizigo kucheleweshwa pamoja na malipo makubwa katika kupitisha bidhaa za maonesho. “Maonesho si biashara, bali ni njia ya kujitangaza hivyo serikali ziungane zaidi kuona namna bora ya kuwafanya ili watu wake wafurahie zaidi jumuiya hii (EAC),” alisema.

Washiriki wengine kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Congo na Uganda walitaka kuondolewa kwa vikwazo kadhaa vikiwamo vizuizi vya barabarani wakisema vinawachelewesha. Mratibu wa maonesho hayo, William Rutha aliipongeza serikali kwa kutoa fursa kwa sekta binafsi kuonesha ubunifu.

Alisema maonesho hayo yaliyofunguliwa Juni 26, mwaka huu yatahitimishwa Julai 10, 2022. Alisema maonesho hayo ni matokeo ya makubaliano kati ya Uongozi wa Mkoa wa Kagera na Ofisi ya Waziri Mkuu kufuatia Wiki ya Uwekezaji iliyofanyika Kagera mwaka 2019.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live