Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washauriwa kutumia mbegu za asili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Mbeguuu Mbeguuu.png Washauriwa kutumia mbegu za asili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima nchini wameshauriwa kutumia mbegu za asili zilizofanyiwa utafiti katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ofisa Kilimo Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Rose Massawe ametoa ushauri huo hivi karibuni katika warsha ya wadau wa kilimo ikolojia iliyofanyika jijini Dodoma ambayo iliandaliwa na mradi wa Mkulima Mbunifu kupitia Shirika la Kilimo endelevu Tanzania (SAT).

Massawe amesema wakulima pia wanapaswa kushirikiana na watafiti wa kilimo ili kuwasaidia kupata mbegu bora za asili ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Amesema ni muhimu wakulima wa kupata taarifa sahihi za kilimo ikolojia ikiwemo matumizi ya mbegu bora za asili ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Awali akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Janet Maro alisema warsha hiyo ni muhimu kwa wakulima na wadau wa kilimo ikolojia nchini.

Amesema warsha hiyo inasaidia kupata mrejesho juu ya kilimo ikolojia na jinsi ya kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya kilimo ikolojia.

Naye Mratibu wa program wa taasisi ya biovision Africa Trust ya nchini Kenya, Fredrick Ochieng amesema warsha hiyo imekuwa ni muhimu kwani wakulima wameweza kupata elimu zaidi ya kilimo ikolojia na kujua huduma ambazo zinapatikana.

Ochieng amesema kilimo ikolojia au kilimo hai kimeweza kuboresha maisha ya wakulima wengi kwa kupata faida ya mazao yao na lishe bora.

Amesema kilimo cha kisasa sio rafiki kwa afya za watu, kwani huchangia magonjwa ya binaadamu kudhoofisha ubora wa ardhi na kuwa tegemezi.

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja Mradi wa Mkulima Mbunifu, Erica Rugabandana amesema huduma za mkulima Mbunifu zimepanuka na kuwafikia zaidi ya wakulima 100,000 kupitia majarida na kupitia mawasiliano ya simu.

"Tumekuwa tukipokea ujumbe wa simu na kupokea ujumbe kutoka kwa wakulima wengi ambao wanasoma majarida ambayo yanatolewa bure," amesema.

Rugabandana amesema pia maofisa wa halmashauri wamekuwa wakipatiwa majarida hayo katika wilaya nane ambazo zipo katika mradi, ambao inatekelezwa katika halmashauri za mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida, Tanga na Manyara .

Mkulima wa kilimo ikolojia, Penina Nnko wa Halmashauri ya Meru, amesema kilimo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwao na wamekuwa wakinufaika sana na elimu kupitia jarida la Mkulima Mbunifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live