Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Washauri udhibiti wa madini uongezwe

7f71ffd612941d86a7d723c100265d76 Washauri udhibiti wa madini uongezwe

Wed, 27 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wachambuzi wameishauri serikali iongeze udhibiti wa madini kutokana na utata unaoendelea kuhusu madini ya rubi yaliyopo Dubai.

Katika kipindi cha takribani wiki moja kumekuwa na utata kuhusu jiwe la rubi linalosemekana lilisafirishwa kinyemela kutoka Tanzania kupelekwa Dubai.

Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema jana kuwa, madini ni moja ya rasilimali kubwa za Tanzania ambayo yakisimamiwa vizuri uchumi utakuwa kwa haraka.

Alisema Bara la Afrika likiwekwa pamoja misaada yote na uwekezaji wote, bado bara linapeleka nje Dola za Marekani zaidi ya bilioni 1.82 na kuongeza kuwa Afrika inapeleka rasilimali nyingi nje kuliko inavyopokea.

“Kwa maana hiyo unakuta ni mshangao, nchi za Afrika ambazo zina umasikini mkubwa cha ajabu ndizo zinazotoa mali nyingi kwenye nchi nyingine. Serikali iwe macho zaidi katika kusimamia rasilimali yetu ya madini,” alisema Profesa Moshi.

Alisema endapo itabainika kuwa rubi iliyopo Dubai ilitoroshwa au kuibwa kutoka Tanzania, itakapopigwa mnada serikali ihakikishe Tanzania inapata mgawo wa zaidi ya asilimia 95 ya fedha itakayopatikana.

Wakili wa kujitegemea, Onesmo Mpinzile alisema pamoja na kuwa Tanzania ina sheria inayoruhusu usafirishaji wa madini nje, lakini utaratibu wa kuyawekea alama ili kujua yametoka wapi haupo.

Alisema nchi kama Japan wanawekea alama madini yao kitu ambacho ni rahisi kuyafuatilia popote duniani lakini kwa Tanzania utaratibu huo haupo.

“Sasa kusema kwamba madini ukubwa ule yanaweza yakaenda bila kujulikana ni ya nani si jambo jepesi, ni jambo linalohitaji uchunguzi, kwa hiyo mamlaka za ndani kwa kushirikiana na Tume ya Madini zichunguze,” alisema Mpinzile.

Mtaalamu na mfanyabiashara wa vito wa Marekani ambaye aliwahi kutembelea Tanzania, Jeffery Bergman alisema kuna taarifa zisizo sahihi kuhusu rubi iliyopo Dubai inayosemekana kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 120.

Alisema rubi ya Winza haipo kwenye rangi ya kijani labda imetoka Longido na wala haikaribii ukubwa wa rubi iliyowahi kupatikana duniani kwa kuwa ana mifano ya rubi zilizofikia uzito wa kilo 44 na kilo 45.

“Kuhusu thamani inayodaiwa ya Dola za Marekani milioni 120, huu ni upuuzi. Bei ya soko ya rubi kubwa ya kijani ya kilo 2.8 ni takribani Dola za Marekani 350 kwa kilo na hivyo kufanya thamani halisi kuwa takribani Dola za Marekani 1,000. Inaonekana kama vile wamiliki walitaka kumrubuni mtu tajiri kwa madai yao ya uongo,” alisema Bergman.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live