Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasafishaji madini safari za nje sasa kukoma

694f518785dd83083f0bad4019bc190c Wasafishaji madini safari za nje sasa kukoma

Mon, 19 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imebainisha kuwa kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza Precious Metals kwa asilimia 99.99 kiko katika kukamilisha taratibu za ufunguzi wake mwezi huu.

Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku.

Akizungumza baada ya semina ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya madini nchini, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kwa sasa kuna viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu kwa asilimia 99.99.

Alisema viwanda hivyo viko katika mikoa ya Geita ambacho kina uwezo wa kusafisha nusu tani, Mwanza (kilo 480) na cha Dodoma uwezo wake ni kilo 50 kwa siku.

Waziri huyo alisema kufanikiwa kwa kiwanda hicho kutafanya madini hayo kuwa chanzo cha malighafi kwa viwanda vya nchini na hivyo kusafirisha dhahabu ikiwa tayari imesafishwa.

"Kukamilika kwa kiwanda hiki kitafanya hata bei ya dhahabu kupanda kwa sababu itakuwa imesafishwa kabisa na itauzwa kwa bei ya mwisho kabisa,"alisema.

Biteko alisema pia kukamilika kwa kiwanda hicho kitachangia ongezeko la ajira.

"Hata ajira zitatokea hapa, kwa mfano kiwanda cha Mwanza kinatarajiwa kutoa ajira 100 kwa awamu ya mwanzo."

"Pia teknolojia ya usafishaji haikuwepo nchini tangu nchi ipate uhuru na kwamba yalikuwa yakipelekwa Dubai na Swaziland kwa ajili ya usafishaji lakini sasa itasafishwa hapa nchini na hivyo manufaa ni makubwa."

Alisema kiwanda cha Mwanza ambacho kinaendeshwa kwa ubia kati ya wawekezaji wa nje na ndani kimekamilika na kwamba ndani ya Aprili mwaka huu taratibu zote za kukifungua zitakamilika.

"Mpaka sasa yameshafanyika majaribio na tumepata matokeo mazuri sana na baada ya muda tunaanza kusafirisha dhahabu zetu zenye muhuri wa Tanzania nje ya nchi."

Kwa upande wa kanuni zilizowasilishwa katika semina hiyo, Biteko alisema miongoni ni inayosimamia Taasisi ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesiasilia (TEITI) ambapo kama nchi imepiga hatua kubwa katika kufikia vigezo.

Alisema awali kulikuwa na vipengele 18 ambavyo Tanzania ilikuwa haijakidhi lakini hivi sasa vimebakia saba ambavyo vinakinzana na sheria za nchi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula alisema kuzijengea uwezo kamati hizo inaipa uwezo mzuri wa kusimamia sekta na serikali vizuri.

"Tumeridhika kanuni hizi zinakidhi matarajio, yako marekebisho madogo madogo yanahitajika lakini hayawezi kuathiri utendaji na usimamiaji wa sekta husika ya madini,"alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz