Wasafirishaji, wachumi na wananchi mbalimbali wamepongeza ahadi ya serikali ya kuweka ruzuku na kupunguza au kuondoa tozo mbalimbali kwenye mafuta ili kuleta nafuu ya maisha kwa wananchi.
Hivi karibuni serikali ilitangaza kuweka ruzuku ya Sh. bilioni 100 kwenye mafuta na kurekebisha au kuondoa kodi na tozo mbalimbali katika bajeti ya serikali itakayowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Juni 16, mwaka huu.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mustapha Mwalongo, alisema wanaziona juhudi hizo kuwa zinakwenda kukabili na kupunguza mfumuko wa bei ya mafuta, na kwamba kwa sasa wamekaa mkao wa kusubiri siku 25 zijazo.
“Juhudi za serikali tunaziona, ndiyo maana unatuona kwa muda sasa tupo kimya, serikali imeamua kutia mkono kama maombi yetu ya awali tuliyozungumza nao tukiitaka iingilie kati ili kuleta ahueni,” alisema.
Aliongeza kuwa wanajisikia faraja kuona kuwa serikali imeamua kuyafanyia kazi maombi yao waliyoyatoa na wanaamini kuwa mafuta hayo yatashuka bei ifikapo Juni au Julai, mwaka huu.
“Kwa hiyo tunaiomba serikali iendelee kutia jitihada, juu ya suala la mafuta kwa kuwa katika biashara hii ya usafirishaji mafuta ndiyo uti wa mgongo. Tunaishukuru kwa hapa ilipofikia tunaridhika sana,” alisema Mwalongo.
Naye Mwenyekiti wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam, Sabri Mabrouk, alisema wanafurahi kuona serikali inajituma na kwamba wanasubiri ahadi hiyo kwa hamu kwa kuwa wanaamini mafuta yakishuka yatasaidia kurudisha hesabu ya zamani ambayo ilikuwa inatoa faida.
“Unajua sisi wa daladala tulianza kuathirika tangu zile ‘level seat’ (kutosimama abiria) za kipindi cha corona, hatukupumzika sana ikaja vita ya Ukraine ambayo imesababisha hii adha ya mafuta, kwa hiyo jitihada za serikali kupunguza mafuta ni nzuri na tunazisubiri kwa hamu kwa kuwa bado tunafanya biashara kwa hasara,” alisema Mabrouk.
Aliongeza kuwa jitihada hizo za serikali pia zinaonyesha ni jinsi gani inawafikiria wananchi wake kwa kuwa adha hiyo pia imewaathiri watumiaji wa magari hayo hasa wanaopanda daladala.
“Kama unatumia daladala dada yangu utaona jinsi zilivyopungua barabarani kutokana na wamiliki wengi kuamua kulaza magari, hali hii ikiendelea itasababisha usafiri wa abiria kuwa wa shida hivyo kuathiri shughuli za wananchi zinahitaji huduma hii, kwa hiyo tunaishukuru serikali kwa kuliona hili,” alisema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Hoseana Lunogelo, alisema kuwa jambo litakuja kwa wakati muafaka kwa kuwa maeneo mengi kutakuwa na shughuli za mavuno, hivyo kushuka kwa bei kutasaidia bei ya vyakula isipande.
“Kwa sasa serikali imefanya jambo kubwa la kuhakikisha kuwa mfumuko hauendelei na baada ya muda tunategemea bei hizo zitashuka hali ambayo inaleta faraja, ukizingatia tunaelekea kipindi cha mavuno sasa bei hizo zikiendelea kupanda hata kupatikana kwa mavuno shambani kusingesaidia kushusha bei ya chakula kwa kuwa gharama za kusafirisha zingekuwa juu,” alisema.
“Kuna sekta nyingine zilikuwa bado hazijaambukizwa kwenye hili tatizo la mfumuko, kwa mfano gharama za hospitali, shule sasa kama serikali isingechukua hatua za kusitisha mfumuko wa bei hata huku pia kungekuja kuambukizwa, naipongeza kwa hili,” alisema mchumi huyo.
Meneja wa kampuni ya mabasi ya Tashrif, Shabani Shemweta, alisema jitihada za serikali kupunguza bei ya mafuta zitaokoa vijana waliokosa kazi kwa kuwa wamiliki watarudisha mabasi waliopaki kutokana na changamoto hiyo.
“Kuna vijana wamepoteza kazi wapo mitaani wanaumia kutokana na uamuzi wa wamiliki kupunguza ruti za magari ili kufidia gharama za mafuta, sisi tunaishukuru serikali yetu kwa kuendelea kutupigania katika suala la mafuta kwa kuwa bado ni changamoto katika sekta ya usafirishaji. Japokuwa nauli zimepandishwa, lakini bado faida haipatikani kwa sababu hela yote inaishia kwenye mafuta na kulipa dereva na kondakta,” alisema.
Kondakta wa daladala zinazokwenda Kawe, Aziz Juma alisema kuwa juhudi zinazofanywa na serikali za kupunguza bei ya mafuta ni za kiungwana na zinaonyesha ni jinsi gani inavyojali watu wake, hasa madereva na makondakta waliopoteza ajira kutokana na wamiliki wa daladala hizo kusimamisha huduma hiyo.
“Yaani dada mimi hapa naisubiri hiyo ahadi ya kushuka kwa bei ya mafuta kwa hamu kwa sababu ninaamini madereva waliopo mtaani watarudi kazini, kwa kweli hii ndiyo serikali tunayoitaka, inayotafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoumiza wananchi,” alisema.
Naye Doris Peter, mkazi wa Ubungo External, alisema kuwa jitihada za serikali za kudhibiti na kupunguza mfumuko wa bei ya mafuta ni za kupongezwa kwa sababu wananchi wa hali ya chini ndiyo wanaumia zaidi, kwasasa pikipiki na bajaji zimepandisha bei.
“Kwa kweli mimi huyu mama (Rais Samia) nina mpenda sana, anajua kufikiria watu wake, sisi ambao tunalazimika kupanda bajaji au bodaboda kutokana na umbali wa kufika kituoni tunaiona joto ya jiwe, naitamani sana hiyo siku ambayo bei ya mafuta itatangazwa kuwa imeshuka, ili turudi katika maisha ya zamani, maana sasa kila kitu kipo juu,” alisema Doris.
TOZO/KODI
Hadi sasa tozo zinazotozwa kwenye mafuta ni ya matumizi ya miundombinu ya bandari inayotozwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuchakata nyaraka za forodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupima na kuthibitisha kiwango cha mafuta kinachopokelewa nchini ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).
Kupima na kuthibitisha ubora wa mafuta ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), uwakala wa Meli ya Shirika la Wakala wa Meli (TASAC) na ya shughuli za udhibiti wa biashara ya mafuta ya EWURA.
Aidha, tozo za taasisi za serikali ni matumizi ya bandari, huduma kwenye halmashauri, tozo katika biashara ya jumla na rejareja kwa wakaguzi wa miundombinu, Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC), OSHA, Zimamoto, Wakala wa Barabara Tanzania (TANDROADS), Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA).
Mei 10, mwaka huu, Waziri wa Nishati, January Makamba, aliwasilisha bungeni hatua zilizochukuliwa na serikali ili kuleta nafuu.