Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasafiri wa mwendokasi walia kusota vituoni

46236 Mwendokasipic Wasafiri wa mwendokasi walia kusota vituoni

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watumiaji wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka au mwendokasi wamesema wanalazimika kutumia wastani wa saa moja au moja na nusu kusubiri usafiri huo licha ya kuwahi vituoni wakati wa asubuhi.

Wameeleza hayo leo, Jumanne Machi 12, 2019 katika kituo kikuu cha mabasi cha Kimara wilayani Ubungo wakati wakizungumza na Mwananchi kuhusu mwenendo wa usafiri huo wenye changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa mabasi.

Danny Rweyemamu aliyekuwa akisubiria usafiri huo amesema amefika kituoni hapo tangu saa 12 asubuhi lakini hakufanikiwa kupata usafiri kutokana na mabasi kufika yakiwa yamejaa.

"Hadi muda huu saa moja inakwenda na robo sioni dalili ya kupata usafiri hali ni mbaya kwenye mwendokasi sielewi cha kuongea ila mamlaka husika zitueleze tunaotumia mabasi haya. Likitokea gari basi shughuli inakuwa pevu hadi ulipande ni kazi kwa wingi wa abiria uliopo hapa," amesema  Rweymamu.

Naye Mwamini Liston amesema suala kusubiri gari saa 1 au karibia mbili ni jambo lililoanza kuzoeleka kwa sababu hawana namna ya kuliepuka isipokuwa mamlaka husika kuingilia kati.

"Unadamka asubuhi kuja hapa, lakini unachokikuta hapa Mungu mwenyewe anajua. Watu wanachelewa kazini, shuleni hadi katika vibarua kutokana na adha hii," ameeleza Mwamini.

Kwa upande wake, Edwin Makingi amesema "Huu si mwendokasi bali ni mwendo wa kukaa vituoni kwa muda mrefu tukisubiri usafiri wa kwenda maeneo mbalimbali. Si siri tunapata shida watumiaji wa usafiri hadi tunasema tumekosea nini sisi watu wa Kimara hasa baada ya kuondoa zile daladala," amesema Makingi.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz