Kamati ya ulinzi na usalama ya Manispaa ya Wilaya ya Bukoba imeombwa kuziwajibisha taasisi za kifedha ambazo zimekuwa zikijihusisha na mikopo umiza maarufu kama kausha ‘damu’ ambazo baadhi hazijasajiriwa.
Ombi hilo lilitolewa na Naibu Meya wa manispaa hiyo, Mwajabu Galiatano Agosti 30, 2023 wakati wa kikao cha baraza la madiwani baada ya kuhoji ni lini manispaa hiyo itaanza kupiga marufuku mikopo hiyo.
Galiatano amesema baadhi ya familia ambazo zimekuwa zikijihusisha na mikopo hiyo baba au mama wamekimbia familia zao huku wakiacha watoto wao hawana mahitaji muhimu.
“Mikopo kausha damu imesababisha baadhi ya wanafamilia kuzikimbia familia zao na kusababisha watoto wanapotoka shule kukosa chakula na mahitaji mengine ya nyumbani kutokana na mzazi kunyangaywa kila kitu ndani ya nyumba na watoa mikopo hiyo baada ya mzazi kushindwa kulipa,”amesema Galiatano
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Renatus Mutatina ameviomba vyombo vya dola kushughilikia jambo hilo haraka iwezekanavyo.
Mkuu wa polisi Wilaya ya Bukoba, Bashir Bashir amesema watalifanyia kazi kwa kuangalia mazingira ya utoaji wa mikopo hiyo huku akiwaomba madiwani kutoa elimu kwa wananchi wao na kuwashauri kuomba mikopo katika taasisi za fedha zenye riba nafuu.