Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waomba benki ikopeshe Kacu kinunue tumbaku

065bc704ab60de66fa6b757fb7c7c454 Waomba benki ikopeshe Kacu kinunue tumbaku

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WANACHAMAwa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (Kacu) wameziomba taasisi za fedha kukipa mikopo vchama hicho ili kinunue zao la tumbaku kwa msimu wa mwaka 2021/2022 na kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.

Waliyasema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa 25 wa chama hicho huku wakilalamikia zao la tumbaku kuwapa hasara.

Baadhi ya wajumbe Makenzi Nkunda kutoka Amcos ya Jitegeme na Joseph Nganiki kutoka Amcos ya Saweka walisema katika kipindi cha mwaka jana, zaidi ya kilo 2000 za tumbaku zilikosa mnunuzi hali iliyowalazimu wakulima kupata hasara kutokana na zao hilo kununuliwa kwa bei ya ndogo.

"Tunaziomba taasisi nyingine za kifedha nchini, kutoa mikopo kwa Kacu ili kinunue tumbaku kwa msimu wa kilimo wa mwaka huu; wakulima tunazalisha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, lakini mwisho wa siku tunakosa masoko… Hili ni tatizo kubwa," alisema Nkunda.

Mintarafu suala hilo, Nganiki alisema kila mwaka wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikumbana na tatizo la kukosa soko ama kukosa wanunuzi hali ambayo inawakatisha tamaa kuendelea kulima zao hilo linaloliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

"Endapo Kacu itaanza kununua tumbaku, tutaondokana na tatizo la wakulima kukosa wanunuzi pindi wanapotaka kuanza uzalishaji, benki zetu zitusaidie kutatua changamoto hii maana kule vijijini watu wanapata shida sana baada kulima na kukosa mnunuzi," alisema Nganiki.

Meneja wa Kitengo cha Kilimo na Biashara wa Benki ya CRDB, Richard Tarimo, alisema benki hiyo inaendelea kutoa mikopo kwa vyama mbalimbali vikiwamo vya msingi nchini.

Alisema katika msimu uliopita, CRDB ilitoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 30 kwa wakulima wanaozalisha tumbaku.

Mwenyekiti wa Kacu, Emmanuel Charahani, alisema wazo hilo watalifanyia kazi kwa ukaribu, lakini muda si mrefu chama hicho kitazindua kampuni mpya ya ushirika itakayojiendesha kibiashara, hivyo wakulima hao wasiwe na wasiwasi.

"Kampuni yetu mpya tumelenga kuiendesha kibiashara ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa ufanisi mkubwa miradi yote inayotekelezwa na KACU sambamba na kutoa ajira kwa wakulima wetu,"alisema Charahani.

Chanzo: habarileo.co.tz