Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wapewa mbinu mikopo bila riba

519e74f3c83b483dd969f55704f1f143 Wanawake wapewa mbinu mikopo bila riba

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mratibu wa Umoja wa Wanawake wa Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Dk Ave-Maria- Semakafu amehimiza wanawake warasimishe vikundi vyao na kuanzisha majukwaa ya kiuchumi ili wapate mikopo bila riba iliyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Dk Semakafu alitoa wito huo mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Chuo cha Mtakatifu Joseph, Ubungo, Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na vikundi vya maendeleo vya wanawake vilivyoko chini ya Shirika la Mabinti wa Maria Immakulata (DMI).

Mikopo hiyo ni tofauti na ile inayotolewa na halmashauri na manispaa na halmashauri zote nchini kupitia asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.

Dk Semakafu alisema mikopo hiyo ni muhimu katika kuwainua wanawake kiuchumi na kutoka katika biashara ndogo na kuingia katika biashara kubwa ukiwemo uzalishaji kupitia sekta za kilimo na viwanda.

“Nilimsikia Rais Samia akiongelea uundwaji wa majukwaa ya wanawake kiuchumi, hii ni fursa adimu kwetu. Katika kuunda majukwaa wanawake tutajisimamia, si mmesikia kuna ‘pochi la mama’ limefunguliwa kila mkoa.”

“Lile pochi (mkopo wa fedha) utaweza kuligusa kama upo katika vikundi rasmi, haya majukwaa ni ufunguzi mzuri kwetu kina mama. Sasa twendeni kwenye majukwaa yetu tukiyaunda tuyasajili kwa ajili ya mchakato huu,” alisema.

Dk Semakafu alisema si kila mtu anaweza kunufaika katika mfumo huo wa utoaji mikopo kwa wanawake, bali ni wale waliopo kwenye mfumo rasmi na kusajiliwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James ambaye alimwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema Siku ya Wanawake Duniani inaikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa wanawake na kuondoa mtazamo hasi dhidi ya kundi hilo.

Aliitaka Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Ubungo kuhakikisha kikundi cha wanawake wa DMI kinasajiliwa ili kipate fursa ya kupata mikopo hiyo na kuwaonya maofisa watakaoleta urasimu katika zoezi hilo.

Mwenyekiti wa Wanawake wa DMI, Isabella Maembe alisema lengo la kuanzisha umoja huo mwaka mwaka 2003 ni kumkomboa mama na mtoto pamoja na kuwawezesha kiuchumi kupitia shughuli za maendeleo.

“Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, DMI imeweza kufikia mitaa 15 ikiwa na wanachama 1,200 kupitia programu yake ya maendeleo ya jamii. DMI imejitolea kuwapenda na kuwatumia watu wote wenye uhitaji hasa wanawake na watoto ili kuwawezesha kupata maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Maembe.

Akizungumza katika kilele cha Siku ya Wanawake Duniani mjini Unguja, Zanzibar, Rais Samia alisema serikali ipo katika mchakato wa kutoa mitaji kwa wanawake bila riba, lengo likiwa ni kuwawezesha kuinuka kiuchumi.

Alisema tayari serikali imeshafanya mazungumzo na benki za CRDB na NMB ili kuandaa dirisha maalumu kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live