Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake wahimizwa kujitosa katika uvuvi

Meli  Uvuviii.png Wanawake wahimizwa kujitosa katika uvuvi

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amewataka wanawake kuingia moja kwa moja kwenye sekta ya uvuvi badala ya kuwategemea wavuvi kupata samaki.

Profesa Mdoe amesema hayo leo Desemba 5, 2023 wakati akifungua warsha ya kikanda ya mafunzo kwa vikundi, ushirika na vyama vya kinamama katika uvuvi mdogo Afrika iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (FAO).

"Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanzishwa BBT kujenga maisha bora kupitia mifugo na uvuvi, Serikali imetoa fedha kuwasaidia kinamama kwenye uvuvi,” amesema Profesa Mdoe.

"Miezi miwili iliyopita tulizindua mradi wa kutoa boti kwa mkopo. Boti hizi tunakopesha kupitia vikundi, ni wakati sasa wanawake wajiunge kwenye vikundi wafanye biashara ya uvuvi moja kwa moja."

Amesema Serikali inagawa boti hizo 160 zilizojengwa kwa Sh11 milioni kwa wanawake na vijana kupitia vikundi pekee.

Akizungumzia mkutano huo uliowakutanisha wanawake waliopo kwenye sekta ya uvuvi ndani na nje ya nchi, Profesa Mdoe amesema ni fursa ya kutengeneza mtandao wa wanawake kuwa na nafasi kwenye ujenzi wa uchumi wa buluu.

Fursa nyingine kwenye mkutano huo unaojumuisha wanawake kutoka zaidi ya nchi 20 za Afrika na Asia ni kubadilishana uzoefu na kujenga mtandao wa biashara.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkaazi wa FAO Tanzania, Nyabenyi Tipo amesema warsha hiyo ni fursa ya kuimarisha umoja baina ya wanawake kwenye vikundi vya uchakataji na wachuuzi wa samaki kwenye kanda.

Amesema wamefanya utafiti na kubainisha changamoto zinazowakabili wanawake kwenye mnyororo wa thamani wa dagaa mkoani Kigoma.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya maendeleo ya wanawake nchini Uganda, Katosi Development Women Trust (KWDT), Magret Nakato amesema kuna wanawake wengi wanaingia kwenye uvuvi lakini kikwazo kikubwa ni mtaji.

"Kuna kikwazo kinatufanya tusionekane kwenye majukumu yetu, suala la mtaji ni lazima lishughulikiwe ili tuzibe pengo na kuwapa wanawake nafasi ya kuonyesha mchango wao kwenye uchumi wa buluu,” amesema.

Amesema asilimia 47 ya waofanya uvuvi Afrika ni wanawake na asilimia 90 ya wanawake kwenye mataifa yanayoendelea wanafanya shughuli za uchakataji.

Dilo Francis, mchakataji wa samaki katika Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma, amesema ni muhimu wanawake kuwekeza kwenye teknolojia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live