Wauzaji na mawakala gesi wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na mizani ya kupimia kiwango stahiki cha gesi kama sheria inavyoagiza.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Vipimo Mkoa wa Lindi, Andrew Mbwambo Machi Mosi, 2023 katika semina ya wadau wa gesi.
“Ni kosa kisheria kuuza gesi bila kuwa na mizani kwahiyo mnapaswa kuhakikisha mnakuwa na mizani ili kuepuka hatua Kali za kisheria kwa wale watakaobainika kutokuwa na mizani huku akitoa siku 14 kwa wale ambao hawana mizani," amesema Mbwambo.
Amesema bado wapo baadhi ya wafanyabiashara wanaouza mitungi ya gesi bila kupima kitu ambacho ni kinyume na sheria kwani uzito unatakiwa kuonekana kabla ya mtumiaji wa mwisho hajaanza kutumia.
Amesema ni vyema mtumiaji wa gesi akaona na kuhakikisha muuzaji akiwa amepima na amejiridhisha kabisa kuwa ni kiwango stahiki na kama ni pungufu anaona.
Amesema kuwa endapo wauzaji wa mitungi ya gesi watafuata sheria malalamiko ya wananchi juu ya ujazo hafifu yataisha na kuwataka wafanyabiashara kuwa waaminifu katika kazi zao.
Hasani Mkupete ambaye mni wakala wa gesi Lindi amesema kuwa pamoja na changamoto za mizani iliyopo lakini wanaomba mawakala vipimo kuwatembelea wauzaji mara kwa mara ili kuwapa elimu umuhimu wa matumizi ya mizani hizo.
Semina hiyo ya wafanyabiashara, wauzaji na mawakala imeandaliwa na Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Lindi lengo kuwapa uelewa umuhimu wa matumizi ya mizani.