Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaolalamika kukadiriwa kodi kubwa waitwa TRA

36435 Pic+tra Wanaolalamika kukadiriwa kodi kubwa waitwa TRA

Sun, 13 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabishara wanaohisi kukadiriwa kiasi kikubwa cha kodi kutoishia kunung’unika na badala yake wafuate taratibu ili malalamiko yao yafanyiwe kazi.

Mamlaka hiyo imesema haina dhamira ya kukomoa watu bali inataka kukusanya kile ambacho Serikali inastahili kupata kihalali.

Hayo yalielezwa na mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam jana.

“Kumekuwapo malalamiko ya wafanyabishara wadogo wanaokadiriwa kodi kwa kile wanachodai wanaonewa lakini hawachukui hatua kutafuta ufumbuzi wa hilo.

“Hatuna lengo la kumkomoa mtu tunataka Watanzania wote wawajibike kulipa kodi kulingana na wanachokiingiza bila kuiibia Serikali wala mlipa kodi.”

“Sasa kama unahisi umekadiriwa kiasi kikubwa tofauti na biashara yako usiishie kunung’unika fika ofisini kwetu uwasilishe malalamiko yako, zipo hatua mbalimbali za maamuzi,” alisema.

Kayombo pia alisisitiza umuhimu wa kudai risiti ili kukabiliana na wafanyabishara wanaocheza michezo michafu kwa lengo la kukwepa kodi.

“Ifike wakati Watanzania wagome kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wanaokwepa kodi, yaani ukienda dukani hataki kukupa risiti unaacha kununua huendi tena, tukiwa na msimamo huu wenyewe watabadilka.” “Na wewe mnunuzi hakikisha unapata risiti maana huo ndio uthibitisho wako endapo litatokea lolote, kama haifahamiki niwaeleze kuwa ukikutwa na mali isiyo na risiti faini yake ni kuanzia Sh30,000 hadi Sh1.5 milioni kulingana na thamani ya ulichonunua,” alisema.

Kwa upande wake, kaimu mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dk Benard Archiula alisema ni muhimu kwa Watanzania kufahamu umuhimu wa kulipa kodi na kufanya jambo hilo kwa hiyari.

“Shughuli nyingi za Serikali zinategemea kodi tunazolipa, hivyo kama tunataka maendeleo hatuna budi kulipa kodi na kuwa sehemu ya maisha yetu,” alisema Archiula.



Chanzo: mwananchi.co.tz