Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaoingiza maziwa nchini wasakwa

MAZIWA Wanaoingiza maziwa nchini wasakwa

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ametoa mwezi mmoja kwa maofisa wa serikali kuwasaka na kuwakamata watu wanaojihusisha na uingizaji wa mazao ya mifugo nchini, ikiwamo maziwa na kuwachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maziwa yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma kwa njia ya kielektroniki, Waziri Mpina alisema kamwe Tanzania haiwezi kukubali kugeuzwa soko la bidhaa zinazoingizwa kiholela kutoka nje ya nchi, huku akitaka hatua za kuimarisha uwekezaji nchini ziendelee kuchukuliwa.

Alisema suala hilo litasimamiwa kikamilifu na wizara yake ili kuhamasisha viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji na kupunguza uagizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi.

Mpina alimwagiza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS), Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko (DPM), Bodi ya Maziwa (TDB) na Bodi ya Nyama (TMB) kuongeza udhibiti kupitia Operesheni Nzagamba, ili kuzuia kwa namna yoyote uingizaji wa mazao ya mifugo nchini bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Pia aliagiza wanunuzi wote wa maziwa hasa wasindikaji kuzingatia mwongozo uliotolewa na wizara wa kununua maziwa ghafi kwa bei isiyopungua Sh. 800 kwa lita ya maziwa, ili kufidia gharama za uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuchochea uzalishaji zaidi kwa wafugaji.

Kadhalika, aliagiza kuzingatiwa bei elekezi ya Sh. 10,000 kwa uhimilishaji kwa ng’ombe bila vichochezi kama ilivyowekwa katika kanuni.

Alisema kanuni hizo zimetungwa ili kuweka usimamizi thabiti wa uhimilishaji nchini na kuweka bei elekezi ambayo inatoa unafuu zaidi kwa wafugaji badala ya kiwango cha zamani cha zaidi ya Sh. 25,000 kwa ng’ombe.

“Ninaagiza katika kipindi cha miaka miwili ijayo nchi yetu isiagize tena maziwa kutoka nje ya nchi, wadau wote wanaagizwa kuweka mikakati madhubuti kufikia malengo hayo,” alisema Mpina na kuongeza:

“Nchi yetu ina ardhi yenye rutuba, ina malisho bora na mifugo mingi, hatuwezi kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi. Tena wakati mwingine tunaagiza maziwa kutoka nchi ambazo hazina hata mifugo, suala hili halivumiliki tena,” alisema Waziri Mpina.

Alisema wizara imepokea maelekezo kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kupitia Mwenyekiti wake, Mahmoud Mgimwa, kupiga marufuku matumizi ya maziwa ya unga kama NIDO, Lactogen kutoka nje ya nchi katika ofisi za serikali.

Alisema suala hilo litasimamiwa kikamilifu na Wizara ya Mifugo ili kuhamasisha viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji na kupunguza uagizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi.

Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk. Sophia Mlote, alisema wiki ya maziwa imeleta hamasa kubwa kwa wananchi na kumhakikishia Waziri Mpina kuwa atasimamia maelekezo yote ili kuleta mageuzi ya kweli kwenye sekta ya maziwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadau wa Maziwa, Catherine Dangat, aliishukuru serikali kwa hatua inayochukua ya kudhibiti uingizaji holela wa maziwa kutoka nje ya nchi na kuomba udhibiti huo uendelee ili kulinda viwanda vya ndani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live