Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaodanganya kiwango cha uchenjuaji dhahabu matatani

53625 Pic+dhahabu

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wachenjuaji wa dhahabu kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini wataanza kubanwa kuanzia sasa baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu wa uzalishaji.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Waziri wa Madini Dotto Biteko alisema walibaini udanganyifu mkubwa unaofanywa na wachenjuaji ikiwamo kuandika idadi pungufu ya madini ya dhahabu yanayopatikana.

Alisema kutokana na udanganyifu huo waliamua kufanya ukaguzi wa viwango vya dhahabu inayochenjuliwa kwa kuwataka wenye mashine zinazotumika kuchenjua kuwasilisha taarifa zao.

Biteko alisema wamekamilisha uhakika huo na baada ya Pasaka watawaruhusu wale waliokamilisha vigezo kuendelea na shughuli zao.

“Udanganyifu ulikuwa mkubwa, kuna mahali huko Chunya (Mbeya) tulikuta kuna mtu amepata kilo moja na gramu 624, lakini wameandika gramu 208,” alisema waziri huyo.

“Mbali na Chunya, Shinyanga pia tulibaini mtu amepata kilo nne ameandika gramu 51, kutokana na hilo tukaamua kuweka control mechanism (mfumo wa udhibiti) ili kubaini kinachopatikana.”

Alisema ili kuhakikisha wanakuwa na kumbukumbu sahihi, wameongeza watu kwenye maeneo hayo na wao wanapata taarifa za dhahabu inayopatikana, lakini wamewataka wenye mashine nao kuwa na taarifa sahihi.

“Kama Mamlaka ya Mapato (TRA) wanavyofanya, mfanyabiashara ana taarifa zake na wao wana zao, wanapokuja kufanya majumuisho wanatakiwa kuwa na kitu kimoja kinachofanana,” alifafanua Biteko.

Hivi karibuni Serikali iliamua kufanya mapitio ya sera na kanuni kwenye sekta ya madini ambayo inachangia nusu ya mapato yanayopatikana kutokana na mauzo ya bidhaa nje.

Mapitio hayo yanakwenda sambamba na upitiaji wa mikataba ya kampuni kubwa za uzalishaji wa dhahabu nchini.

Serikali pia imezindua Soko Kuu la Dhahabu mkoani Geita lenye huduma zote muhimu lililofungwa kamera 22 ambazo zinaweza kuchukua kila tukio linalofanyika ndani na nje.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa soko hilo, katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema makusanyo ya maduhuli yatokanayo na dhahabu yameongezeka kutoka Sh24 bilioni mwaka 2011 hadi kufikia Sh114.78 bilioni mwaka 2017/2018.



Chanzo: mwananchi.co.tz