Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaobetisha wapandishiwa kodi

9307 BETTING+PIOC TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanaobashiri matokeo ya michezo mbalimbali, hasa ya soka, watalazimika kujipigapiga mifuko zaidi baada ya Serikali kuongeza kodi katika michezo ya kubahatisha.

Hayo yamo kwenye bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2018/19 iliyosomwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

Bajeti hiyo pia imepunguza kodi katika magari na pikipiki zinazotumika katika michezo kwa lengo la kuboresha utalii, hatua ambayo itakuza michezo hiyo maarufu duniani.

Pengine pigo kubwa litakuwa katika ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani katika michezo ya kubashiri mmatokeo ya mechi, maarufu kama betting, na michezo ya kubahatisha ambayo mashine zinazotumika zimeongezewa kodi katika makusanyo.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Dk Mpango alipendekeza Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41 ifanyiwe mabadiliko ya kiwango cha kodi kutoka asilimia 6 ya mauzo ghafi hadi asilimia 10.

“Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali kutoka kwenye sekta ndogo ya michezo hiyo ya kubahatisha,” alisema Dk Mpango.

Kampuni za michezo ya kubashiri zimeibuka kuwa maarufu duniani, zikikusanya fedha nyingi kutoka kwa mashabiki wa michezo mbalimbali wanaobashiri washindi na ambao wanapatia hujivunia mamilioni ya fedha.

Kutokana na kuingiza fedha nyingi, kampuni hizo zimewekeza fedha nyingi katika kujitangaza, zikidhamini klabu kubwa za soka ambazo zina wafuasi wengi.

Moja ya kampuni hizo kubwa ni SportsPesa ya Kenya, ambayo imeweza kuingia mkataba mnono na klabu ya Everton ya England, huku ikishizishika klabu kubwa za soka katika ukanda wa Afrika Mashariki, zikiwemo Yanga, Simba za Tanzania na AFC Leopards na Gor za Kenya.

Kampuni nyingine zinazoendesha mchezo huo hapa nchini ni pamoja na Mkeka, Premier Betting, M-Bet na Soccer Bet, zikiwa sehemu ya kampuni nyingi zinazoendelea kushamiri nchini.

Hatua hiyo ya kuongeza kodi kwa wanaoendesha michezo hiyo ya ubashiri wa matokeo ya mechi inaweza kusababisha gharama za kushiriki pia iongezeke na pia kupunguza kiwango cha zawadi zinazotolewa na hivyo kuathari shughuli zinazotangaza mchezo huo kama udhamini wa michezo, ambao umekuwa mgumu katika ukanda ya Afrika Mashariki.

Wabashiri hushiriki mchezo huo kwa kujaza fomu maalum zinazotolewa kabla ya mechi za maeneo mbalimbali duniani na hutoa kuanzia Sh500 kulinganisha na uwezo wa mtu.

Wengine hushiriki kwa kutumia huduma za mtandaoni, ambako pia kunaweza kukawa na athari za kupunguza idadi ya washiriki wa mchezo huo wenye uraibu.

Pia kampuni hizo zimetandaza matawi yake sehemu kubwa ya nchi na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wanaofanya kazi katika ofisi hizo.

Katika bajeti hiyo, Waziri Mpango pia alipendekeza kufanya marekebisho ya kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye mashine za michezo ya kubahatisha (slot machines) kutoka Sh32,000 hadi Sh100,000 kwa kila mashine kwa mwezi.

Pia alipendekeza kuongeza kiwango cha kodi kinachotozwa kwenye michezo ya kubahatisha (Casino) kutoka asilimia 15 hadi asilimia 18 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi (Gross Gaming Revenue -GGR).

“Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu kiwango cha asilimia 15 kimedumu kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2012,” alisema Dk Mpango.

Mbali na kodi hizo, Dk Mpango pia alipendekeza kuongeza kiwango kodi kinachotozwa kwenye mashine arubaini (Forty Machines Site) za michezo ya kubahatisha kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20 ya mapato halisi ambayo hupatikana baada ya kutoa zawadi.

“Hatua hizi za marekebisho ya michezo ya kubahatisha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 21,198.8 (Sh21.2 bilioni),” alisema Dk Mpango.

Mbali ya hatua hizo za kuongeza kodi, wanamichezo watakuwa na furaha kupata taarifa za msamaha wa ushuru wa forodha kwa pikipiki zinazotumika katika mashindano, kwa mujibu wa Dk Mpango.

Waziri Mpango alisema uamuzi huo unatokana na makubaliano ya mawaziri wa fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Customs Management Act, 2004).

Alipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linalotoa msamaha wa ushuru wa forodha kwenye magari yanayotumika kwenye mashindano ya mbio za magari (rally cars) na kuingiza pikipiki (motorcycles) ili nazo ziweze kupata msamaha huo.

“Hatua hiyo inatarajiwa kuhamasisha mashindano hayo na kukuza sekta ya utalii,” alisema Dk Mpango.

Mashindano ya magari yameanza kufufuka baada ya kufifia kwa muda mrefu. Miaka ya sabini, mashindano hayo yalihusisha nchi zote za Afrika Mashariki. Hata hivyo mchezo wa pikpiki bado haujaenea sana nchini.

Hata hivyo, Dk Mpango hakugusia mpango wa Serikali wa kuwezesha kufanyika kwa mashindano ya Afrika ya vijana yakayofanyika mwakani nchini Tanzania, ingawa suala hilo lilishazungumzwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa ni moja ya vipaumbele vitatu vya Serikali.

Mashindano hayo yatahusisha kuingiza vifaa vingi vya uendeshaji vitakavyohitaji msamaha wa kodi, kwa mujibu wa kanuni za waendeshaji mashindano hayo.

Lakini akizungumza bungeni hivi karibuni, Dk Harrison Mwakyembe alisema maeneo makuu matatu ya kipaumbele kwa Serikali katika michezo ni maandalizi ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 14 (Afcon 2019) ambayo yatafanyika nchini mwakani huku Tanzania ikiwa ndio mwaandaji.

Eneo jingine ambalo litanufaika na bajeti ya mwaka huu ni ujenzi wa eneo la changamani la michezo mjini Dodoma, ambalo pia Serikali ya Morocco ina mkono wake pamoja na kuboresha miundombinu na vitendea kazi katika Chuo cha Michezo cha Malya mkoani Mwanza.

Maeneo mengine ni uboreshaji wa miundombinu ya Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru, Dar es Salaam, ambayo imekuwa ikitumika kwa michezo mbalimbali ikiwemo ile ya kimataifa. Maeneo hayo ndio yatatumia kiasi kikubwa cha fedha kilichotengwa kwenye bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka 2018/2019.

Wadau wafunguka

Kwa vipaumbele hivyo kwa mwaka huu wa fedha, inaashiria kuwa michezo mingine itakuwa kwenye wakati mgumu kupata sapoti ya serikali.

Hatua hiyo inatokana na ufinyu wa bajeti kwani, vipaumbele ama matukio hayo yaliyopangwa kufanyika mwaka huu, yanahitaji fedha nyingi katika utekelezaji wake.

Dk. Mshindo Msola, ambaye ni kocha zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars amesema, bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya michezo haitoshelezi lakini, akawataka wahusika wa wizara hiyo kujiongeza.

“Nimeusoma huo mgawanyo wa bajeti kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pesa ni ndogo sana. Kiukweli haufurahishi hata kidogo kwa sababu tunatakiwa kupambana kuinua soka la vijana. Hawa vijana tunatakiwa kuwalea tangu wakiwa watoto na mikakati yetu ilitakiwa kuanzia huko ili kuja kunufaika hapo baadaye,” alisema Msola.

“Lakini inaonekana bado kuna dhana kuwa michezo ni starehe, lakini tukiwekeza huko basi tutapiga hatua kubwa sana. Vijana wengi wamejikita katika kucheza soka na kufanya uigizaji hivyo, tungewekeza huko zaidi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz