Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi watoa ya moyoni kupanda kwa kodi ya mawigi

64196 Mawigi+pic

Tue, 25 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Serikali ya Tanzania kupendekeza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa nywele za bandia zinazotengenezwa nchini na asilimia 25 kwa zinazoingizwa kutoka nje baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti katika hilo.

Ushuru huo unatarajia kuanza kutozwa Julai Mosi 2019 itakapoanza kutekelezwa bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/20 ya Sh33.1 trilioni ambayo leo Jumanne Juni 25,2019 inapigiwa kura na wabunge wa Bunge la Tanzania.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Jumanne baadhi yao wamependekeza kupigwa marufuku kwa nywele hizo kama ilivyokuwa kwa mifuko ya plastiki kutokana na kutokuwa na faida huku wengine wakidai wanaume ndiyo watabeba mzigo.

Mkazi wa Tabata Jijini Dar es Salaam, Said Mrisho amesema siyo kupandisha kodi tu bali yangepigwa marufuku kama mifuko ya plastiki kwa sababu na yenyewe haziozi.

“Kufanya hivyo pia kutaturahisishia kujua uhalisia wetu kwa sababu hazina umuhimu wowote, wangepandisha kodi mafuta ya kupakaa ningeandamana lakini siyo mawigi,” amesema.

Ramadhani Mgamba amesema kulingana na imani yake mwanamke kujiongezea nywele bandia ni dhambi huku akibainisha wanaotaka vizuri lazima wakubali kudhurika.

Pia Soma

“Urembo gharama lazima wagharamie sasa wakilalamika kusema wanakomoa siyo sawa sababu si jambo la lazima kama ilivyo kwa chakula na sijajua zina umuhimu gani kwa wanawake sababu zamani hazikuwapo na walikuwa wanapendeza,” amesema Mgamba.

Lugano Bwenda amesema kuongezwa kwa kodi katika nywele bandia kutawaathiri wanaume sababu wao ndiyo wanaotoa pesa za kusuka kwa wake zao.

“Ni fahari kwa mwanamke kuhudumiwa na mume wake hata kama ana kipato kikubwa lakini nafasi ya mwanaume iko pale pale kuhakikisha nyumba ina chakula, inapendeza na ni wanawake wawili kati ya kumi ambao wanaweza kujigharamia katika kusuka,” amesema Lugano.

Mkazi wa Tabata Kinyerezi, Rachel Gorge amesema kupandishwa kodi nywele hizo kutawafanya kupunguza kasi ya kuzitumia tofauti na zamani.

“Kuna wengine hawawezi kukaa mwezi bila kusukia nywele hizo nafikiri sasa umefika wakati wa kuzionea huruma pesa badala ya kununulia mawigi tufanye mambo ya msingi,”amesema Rachel.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz