WAKATI utekelezaji wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi kijiji cha Chongoleani Tanga (EACOP) ukitarajiwa kuanza muda wowote,uongozi wa wilaya ya Handeni tayari umeanza maandalizi ya kutoa elimu kwa wananchi wilayani humo jinsi watakavyonufaika na mradi huo pamoja na kuchangamkia fursa za ajira katika mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni,Toba Nguvila amesema kuwa wakati wakisuburi wananchi wa wilaya hiyo kulipwa fidia katika baadhi ya maeneo ili kupisha mradi huo kuanza,wao wakiwa ni uongozi wa wilaya tayari wameanza kuendesha programu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya faida zitakazopatikana pamoja na fursa za ajira .
" Sisi hapa Handeni tayari tumeanzisha programu mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi kutumia fursa za ujenzi ili kunufaika kibiashara pamoja na ajira rasmi na zisizo rasmi kwa kutoa mafunzo semina za utayari na jinsi ya kunufaika".
Ameongeza: "vile vile hapa Handeni kuna maeneo makubwa ya uwekezaji wa hoteli na chakula kutokana tuna zaidi ya tani za chakula milioni moja,hivyo pia wawekezaji wengine wa kampuni ambazo zitafanya kazi katika mradi huo wanakaribishwa kuwekeza hapa ili kuwapa ajira wananchi wetu"
Mradi huo wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,445 unaotekelezwa kwa gharama za Dola za Kimarekani bilioni 3.5 kwa Tanzania unasimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC),mkoani Tanga linapita katika wilaya tano za Tanga, Muheza, Korogwe, Handeni na Kilindi.
Wilayani Handeni bomba hilo linapita urefu wa kilometa 64 na ni eneo ambapo kutajengwa moja ya kambi kubwa za wafanyakazi na fursa za ajira zinazotarajiwa ni za huduma za jamii,(malazi, chakula,afya,maji)ulinzi.