Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Ulanga walipwa fidia uchimbaji madini

8af91de2bb610a88a0e15b4cdbd459b6 Wananchi Ulanga walipwa fidia uchimbaji madini

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi 1,090 wa vijiji vya Mdindo, Kisewe, Makanga na Nawenge vilivyopo kata tatu za tarafa ya Vigoi wilayani Ulanga, Morogoro wameridhia kupisha uwekezaji mkubwa wa uchimbaji madini ya graphite.

Wananchi hao wamelipwa fidia ya Sh bilioni 14.6 kutoka kampuni ya Faru Graphite Corporation.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Alimiya Osman, amesema hayo mjini Mahenge, wakati wa kuanza kurasimisha utiliaji saini na ulipaji fidia kwa walioguswa na mradi wa madini ya kinywe (graphite), ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Ngollo Malenya.

Osman, amesema kazi ya kurasimisha utiliaji saini na ulipaji fidia itaendelea kufanyika kwa siku chache zijazo na itaenda sambamba na ujenzi wa nyumba mpya 300, kwa wananchi kwenye makazi mapya katika mji mpya wa Ndotoyetu uliopo eneo la Idenke, Kijiji cha Mdindo.

Amewasihi wananchi wanaoguswa na mradi huo kutumia vyema elimu ya matumizi bora ya fedha, ambayo wameshapewa na wataalamu, ili wapate matokeo chanya kwao na jamii nzima ya Wilaya ya Ulanga.

Osman amesema mradi huo hadi sasa umegharimu kiasi cha Sh bilioni 70, sawa na dola za kimarekani milioni 30 na unatarajiwa kutumia Sh bilioni 290 kwa ajili ya ujenzi wa mgodi.

Baadhi ya wanufaika na waliopisha uwekezaji huo Theresia Ninhomo na Akiba Mashi, kwa nyakati tofauti wamesema wameona ni ndoto kwa sababu walishakata tamaa hadi walipoona wamekabidhiwa fedha taslimu.

"Wengine hatukuwahi kushika milioni moja, kumi hata ishirini, lakini kupitia mradi huu tumepata tunatarajia itatunufaisha sisi na familia zetu na wana Ulanga pamoja na umri umekwenda, tunafanya miradi ya maendeleo itusaidie wenyewe na jamii yetu, "amesema Theresia.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya ametoa rai kwa wananchi hao kuhakikisha wanatumia fedha wanazopata ikiwa ni fidia kwa uangalifu na faida kwa familia.

Malenya amewataka fedha wanazolipwa fidia wazitumie kukuza uchumi wao binafsi na jamii kwa ujumla na kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha, ili wasitetereke kimaisha .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live