Baadhi ya wadau wa mazingira katika halmashauri ya wilaya Mbozi mkoani Songwe, wamesema wanakwama kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka kupanda miti mitano kwa kila kaya kutokana na kutopatikana kwa miche ya kupanda.
Wananchi hao wameiambia Mwananchi leo Jumamosi Desemba 31, 2022 kuwa wameitikia mwito wa Serikali kuwataka wapande miti kwenye makazi yao lakini wakati mvua zikiendelea kunyesha hawajui wapi watapata miche ya miti ya kupanda.
Mmoja wa wadau hao, Malick Nzowa ambaye pia ni diwani wa kata ya Hasanga wilayani hapa amesema amewahamasisha wananchi katika kata yake lakini kumekuwa na changamoto ya kupatikana kwa miche ya miti.
“Baada ya kuona uhaba wa miche, wakazi wa kijiji cha London wameamua kupanda miche ya miti ya asili ya maeneo hayo bila kusubiri miche kutoka nje ya kijiji chao,” amesema Nzowa.
Maria Athuman, mkazi wa Mlowo amesema miaka iliyopita kila msimu wa mvua unapoanza wanakuwepo watu ambao wameotesha miche ya miti na kuiuza mtaani, lakini mwaka huu hali ni tofauti biashara hiyo haiko na hivyo kuomba idara inayohusika kutengeneza utaratibu ili wananchi wapate miti ya kupanda.
Ofisa misitu wa halmashauri ya wilaya Mbozi, Hamis Nzunda amesema suala la miche ya miti ya kupanda linashughulikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na kuwa hakuna hofu ya upatikanaji wa miche.
Kuhusu zoezi la upandaji miti mwaka huu, Nzunda amesema halmashauri yake inakusudia kupanda miti 1.5 milioni na kwamba tayari miti 2600 imepandwa katika uzinduzi na kuwa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa Songwe kwa kushirikiana na Wakala wa huduma za misitu (TFS) zitaanza kupanda miti kando ya barabara kuu na za mkoa.
Naye meneja wa TFS, Fredy Mgeni akizungumzia suala la miche amesema wapo wadau ambao wamefundishwa kuotesha miche wanapatikana katika maeneo mengi ya wilaya na kuwa miche mingine ipo kwenye taasisi yake na utaratibu umeandaliwa wa namna ya kuipata.