Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi 800 wafunga ofisi, wazuia madini ya chuma kusafirishwa

A1351268b3779703b6c95576a847cb5b.jpeg Wananchi 800 wafunga ofisi, wazuia madini ya chuma kusafirishwa

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wananchi zaidi ya 800 wa vitongoji vinne vya Masanga, Buyumba, Mwamaganga na Mwamapuli katika Kijiji cha Mwanzugi Kata ya Igunga mjini wilayani Igunga mkoani Tabora wamezifunga ofisi nne za vitongoji baada ya kuwatuhumu viongozi wao kushindwa kusimamia rasilimali zao ikiwemo madini aina ya chuma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuzifunga ofisi hizo baadhi ya wananchi hao Elias Lubeta, Rehema John, Ester Julius, Hamisi Kilimba walisema wameamua kuzifunga ofisi hizo baada ya kubaini kuwa wenyeviti wao wa vitongoji wamemruhusu mwekezaji wa Kampuni ya Awadh kubeba mawe ya madini aina ya chuma bila wao kushirikishwa.

Walisema wamekuwa wakiona malori ya tani 30 yakibeba mawe na kuondoka huku wakihesabu idadi ya tripu za mawe ambapo zaidi ya 100 zimeshabebwa na kupelekwa Mkoa wa Dodoma. Lubeta alibainisha kuwa Desemba 16 mwaka huu walifanikiwa kulikamata lori moja likiwa limebeba mawe ya madini ya chuma.

Alisema baada ya kumuuliza dereva wa lori hilo ambaye hawakumtaja jina lake aliwaambia kuwa mawe hayo wanayapeleka mjini Dodoma na baada ya kupewa majibu hayo walimuamuru kuyapeleka mawe hayo katika Shule ya Msingi Buyumba iliyoko Kijiji cha Mwanzugi na baadaye walimuamuru aondoke.

Hata hivyo wananchi hao walisema hawatazifungua ofisi mpaka pale Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo atakapofika kijijini kwao kusikiliza malalamiko yao ya kuliwa hovyo rasilimali zao pasipo wao kunufaika. Kwa upande wake mmiliki wa kampuni hiyo yenye makao makuu yake Dodoma aliyefahamika kwa jina la Awadh Salum Aboud alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alikiri lori la mawe kuzuiliwa na wananchi na mawe kumwagwa kwenye Shule ya Msingi Buyumba.

Alisema amesikitishwa na kitendo cha wananchi kulizuia lori la mawe wakati yeye ana leseni ya madini ambapo alishalipia mrahaba wa Sh milioni 5.6 na kuongeza kuwa pia amechangia Sh 250,000 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi katika kijiji hicho.

Aliongeza kuwa yeye anafahamu taratibu zote za madini ambapo sheria ya madini inamtaka kuwashirikisha wananchi huku akifafanua kuwa alishafanya kikao na wenyeviti pamoja na wajumbe wake ambapo aligharamia gharama zote za kuwalipa wajumbe posho. Hata hivyo hakutaja kiwango cha posho alichokitoa.

Sambamba na hayo mwekezaji huyo alisema suala hilo mkoa na wilaya inajua, hivyo anauachia uongozi wa wilaya kupitia mkuu wa wilaya kwa kuwa anayo imani kuwa suala hilo litashughulikiwa na yeye kupata haki zake huku akidai yeye alishabeba tripu nane za mawe hayo.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Igunga, Robert Mwagala alikiri ofisi za wenyeviti wa vitongoji kufungwa na kusema kuwa wananchi walichukua maamuzi hayo baada ya kuwauliza maswali viongozi hao na kushindwa kutoa ufafanuzi juu ya mwekezaji kubeba mawe pasipo wao kushirikishwa.

Alisema pamoja na yeye kuwaomba wananchi kuzifungua ofisi hizo ili ziweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi lakini waligoma na kufunga wakidai mpaka mkuu wa wilaya afike kijijini hapo asikilize malalamiko yao.

Naye Diwani wa Kata ya Igunga, Athumani Mdoe alisema baada ya kupokea malalamiko hayo alifika katika kijiji hicho ambapo suluhu haikuweza kupatikana huku wananchi wakiendelea na msimamo wao wakimuomba mkuu wa wilaya afike katika kijiji hicho asikilize malalamiko yao.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga, Ally Mkalipa alithibitisha wananchi kulizuia lori la mawe na kusema kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo alifika eneo la kijiji hicho na kukuta wananchi wakiwa wamelizingira lori hilo.

Alisema baadaye aliamuru waliachie, walikubali huku wakidai mawe hayo yabaki Shule ya Msingi Buyumba na kusema kuwa hakuna mwanachi yeyote anayeshikiliwa na jeshi hilo kwa kuwa hawakufanya vurugu yoyote.

Chanzo: www.habarileo.co.tz