Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanakijiji wapewa ardhi walime zabibu

C277f25e0abbc7395c64bdd19be5e616 Wanakijiji wapewa ardhi walime zabibu

Wed, 28 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa (RC) wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameamuru wananchi wanakiijiji wa Mwegamile katika Kata ya Bwigiri wilayani Chamwino, Dodoma wapewe ardhi yenye ukubwa wa ekari 605 iliokuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili waitumie kwa kilimo cha zabibu.

Alitoa agizo hilo wilayani Chamwino baada ya kupokea taarifa na mapendekezo kutoka kwa kamati maalumu aliyoiunda mwishoni mwa Machi mwaka huu.

Aliunda kamati hiyo kutokana na mgogoro wa ardhi ulioibuka kati ya wanakijiji wa Mwegamile, Halmashauri ya Chamwino na mwekezaji wa Kampuni ya Mega Beverages Limited inayozalisha vinywaji vikali inayotaka kuwekeza katika eneo hilo kwa kujenga kiwanda cha mvinyo na kulima zabibu.

Taarifa ya kamati inaonesha kuwa eneo hilo la ekari 605 ambalo ni sehemu ya shamba la ekari 1,622 lililokuwa likimilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino tangu mwaka 1984 na kupewa kampuni kadhaa za uwekezaji zilizoshindwa kuwekeza ndipo likarudishwa katika umiliki wa halmashauri hiyo.

Halmashauri hiyo ilishindwa kuliendeleza na hivyo wananchi wakaanza kujimilikisha na kuanza kulima.

Alisema mgogoro kuhusu shamba hilo uliibuka baada ya halmashauri hiyo kupata mwekezaji Kampuni ya Mega Beverages Limited ili kujenga kiwanda cha kutengeneza vinywaji vikali.

Halmashauri hiyo ilimuuzia ekari 400 kutoka kwenye eneo hilo ndipo wananchi wakapinga na kudai ardhi hiyo ni mali yao wakitaka wapewe ufafanuzi kwanini mwekezaji amepewa eneo hilo.

RC Mahenge alisema kamati hiyo ilipitia eneo lote lenye ukubwa wa ekari 1,622 na kutoa mapendekezo ya mwekezaji huyo kupewa eneo alilolinunua la ekari 400, kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha zabibu na ujenzi wa kiwanda.

Aidha, ilipendekeza wananchi waachiwe ekari 605 ili waendeshe kilimo cha zabibu na halmashauri kubakiwa na ekari 617 kati ya ekari 1,622 zilizopo.

Baada ya maridhiano hayo, Dk Mahenge aliruhusu mwekezaji huyo kuendelea na ujenzi wa miundombinu na maandalizi ya mashamba baada ya kusitisha shughuli hizo ili kupata maridhiano kutokana na kuibuka mgogoro huo.

Aidha alitoa wiki mbili kwa kamati hiyo kufanya tathmini ya eneo la ekari 605 litakalogawiwa wananchi ili kubaini kama kuna watu walikuwa wakilimiliki, sambamba na kufanya tathmini ya watu walioathirika katika eneo alilopewa mwekezaji ili wapewe ardhi kwenye eneo la ekari 605 zilizotolewa kwa wananchi.

“Kamati msimamie kikamilifu kuhakikisha wale walioathirika na eneo alilopewa mwekezaji ndio wapewe kipaumbele katika kupewa eneo lenye ekari 605, pia mpitie kuona kama eneo hilo hakuna wananchi wanaomiliki eneo hilo tusije kutengeneza mgogoro mwingine,”alisema.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa muwekezaji kwani kiwanda hicho kina umuhimu mkubwa kwa jamii kwa kupata ajira na kukiuzia mazao yao katika kiwanda hicho hasa baada ya

Mwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia mgogoro huo, Aroni Kameta, alisema walipewa hadidu za rejea tisa za kutekeleza katika kutatua mgogoro huo na waliwahoji watu katika ngazi tofauti pamoja na mwekezaji huyo ili kupata taarifa zilizowezesha kutoa ushauri huo uliotolewa.

Mjumbe wa kamati hiyo kutoka kundi la wananchi, Gabriel Masinga, alisema kutokana na nchi kusifika kuwa na amani na maridhiano, wameshirikiana na kamati hiyo na kuja na mapendekezo yenye manufaa kwa pande zote tatu yani wananchi, mwekezaji na halmashauri.

Chanzo: www.habarileo.co.tz