Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanakijiji Mtwara waomba kiwanda cha matunda

13298 Pic+mtwara TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Wakazi wa Kijiji cha Kilambo, wilayani Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali iwasaidie kutafuta mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na mazao ya kilimo katika kijiji chao.

Wamesema ni kutokana na kijiji hicho kuwa na matunda na mazao mbalimbali yanayokosa soko na kuwasababishia umasikini.

Wakazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kijiji cha Kilambo Mohamed Mkama, wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, aliyefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha Kilambo, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, mkoani Mtwara jana Agosti 21.

Wamesema kijiji chao kina fursa nyingi za kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao na kutoa ajira kwa vijana.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kilambo, Mohamed Mkama, amesema kuwa kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika masuala ya biashara na uhusiano wa kijamii.

"Watu kutoka Msumbiji wananunua sana chakula na bidhaa nyingine kutoka kwetu lakini tunawauzia bidhaa bila kuongeza thamani hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi wa kijiji chetu na tunakuomba Waziri wa Fedha utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze kunufaika" amesisitiza.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Selemani Kumamba, alimweleza Waziri wa Fedha na Mipango kwamba kijiji chao ni maarufu kwa kilimo cha matunda hivyo wanapendekeza kujengwa kwa kiwanda cha kusindika matunda ili juisi itakayozalishwa katika kijiji chao iwe na soko.

“Waziri sisi ni wakulima wazuri wa matunda lakini matunda yetu wakati wa msimu yanakosa soko, yanaoza na tunayatupa jambo linalotulazimu tukuombe utusaidie kuhamasisha wawezezaji waje wajenge kiwanda cha kusindika juisi katika kijiji chetu ili nasi tuondokane na umasikini," amesema Mzee Selemani Kumamba.

Waziri Mpango, aliwaambia wakazi hao inabidi ufanyike utafiti wa kutosha ili kubaini wingi wa mazao yanayozalishwa na wakulima katika kijiji hicho na vijiji jirani ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa mazao hayo yakiwemo matunda.

"Tukiwa na uhakika huo hata mwekezaji anayekuja tutamwambia kwa mwaka mmoja, kwa wastani, kijiji hiki na vijiji jirani vinazalisha maenbe kiasi fulani, kwa hiyo wazo la kutaka kuwa na kiwanda ni  zuri lakini linahitaji kufanyiwa kazi zaidi" amesema Dk Mpango aliyeambatana na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda.

Dk Mpango, yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine amekutana na wafanyabiashara wa mkoa wa Mtwara pamoja na kutembelea taasisi zilizochini ya wizara hiyo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz