Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanahisa Yetu Microfinance Plc waunda kamati kufuatilia hisa

Yetu Microfinance Plc 780x470 Wanahisa Yetu Microfinance Plc waunda kamati kufuatilia hisa

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WANAHISA katika Benki ya Yetu Microfinance Plc wameamua kuunda kamati kwa ajili ya kufuatilia hatima ya hisa zao kutokana na kutokuwa na imani na menejimenti yao ambayo imeondolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwezi uliopita.

Wamefikia uamuzi wa kuunda kamati hiyo mapema wiki hii katika mkutano ulioitishwa na waliokuwa viongozi wa benki hiyo uliofanyika Msimbazi mkoani Dar es Salaam.

Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine wanahisa waliibua hisia zao za kutokuwa na imani na uongozi wa benki hiyo.

Wanahisa hao walisema kwamba wameamua kuwa na kamati kwa kuwa hawajui mustakabali wa hisa zao baada ya BoT kuhamishia mali za benki hiyo katika benki ya NMB Plc.

“Wengine tunahangaika sana kupata fedha na hicho kiasi cha fedha ambacho tumeweka kama hisa kinaweza kuonekana kuwa kidogo ila kwetu sisi ni kikubwa sana, kingetusaidia kutimiza mahitaji mbalimbali ya familia zetu …ndio maana tunafanya kila linalowezekana tupate stahiki zetu,” alisema Yohana Meshak mmoja wa wanahisa hao.

Waliongeza kuwa wanaamini kuwa benki kuu haiwezi kuwafanyia vitendo vya kuwaonea hivyo wameamua kuwa na subira na kufuatilia wenyewe kwa kina kujua nini kilitokea mpaka hisa zao zikahamishiwa benki ya NMB Plc.

“Viongozi wetu hawaelezi ukweli. Hapa la msingi iundwe kamati ya wanahisa kutoka miongoni mwetu tufuatilie jambo hili kabla hatujalipeleka kwenye mkondo wa kisheria,” alisema Elizabeti Bulimba mwanahisa mwingine kutoka Dar es Salaam.

Mwezi Desemba mwaka jana, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa taarifa kwa umma ikijulisha kuwa Benki ya Yetu Microfinance imeshindwa kukidhi vigezo vya sheria ya fedha nchini.

Imeelezwa kuwa Benki Kuu ilitoa taarifa tatu tofauti kuhusu mwenendo wa benki hiyo lakini hakuna taarifa iliyofanyiwa kazi na menejimenti ya Yetu hadi mwezi uliopita ambapo BoT iliamua kuhamisha mali za benki hiyo na kuzipeleka NMB Plc.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live