Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanahabari waaswa kumulika fursa nyanda za juu

Bot Mby Meneja Uchumi wa BoT tawi la Mbeya akitoa mafunzo

Mon, 14 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imewaasa wanahabari kuibua fursa za kiuchumi zilizopo Nyanda za Juu Kusini na sehemu nyinginezo nchini Tanzania ili kuwafanya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje kuzitumia kwa ustawi wao na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo jijini Mbeya na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Dkt. Bernard Kibesse wakati akifungua Semina ya Benki Kuu kwa Waandishi wa Habari za Biashara, Uchumi na Fedha.

Akitoa hotuba kwa niaba ya Naibu Gavana, Kaimu Mkurugenzi wa Tawi la Benki Kuu Mbeya, Dkt. Nicholaus Kessy amesema Mkoa wa Mbeya na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini yaani Songwe, Njombe, Katavi na Iringa ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo hazijatumika ipasavyo ili kuchangia katika uchumi wa nchi.

“Fursa hizo ni pamoja na ardhi nzuri ifaayo kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hali ya hewa nzuri pamoja na vivutio vingi vya utalii”amesema Dkt. Kessy na kuongeza kuwa waandishi wa habari pamoja na vyombo vyenu mna nafasi ya kuziibua fursa hizo kwa kuzitangaza na kuvutia watalii kufika katika mikoa hii na kuchangia maendeleo ya nchi yetu.

Ametaja vivutio hivyo kuwa ni pamoja na Mbuga za Taifa za Kitulo, Ruaha na Katavi na kuongeza kuwa hazipati wageni wengi kwani hazitangazwi sana hivyo kuwaomba wanahabari kuzitangaza kwa nguvu zote.

“Mkidhamiria kubadilisha hali hii mnaweza kuifanya Kanda hii iwe maarufu kama ilivyo Kanda ya Kaskazini kwa masuala ya utalii’, alisisitiza Dkt. Kessy.

Akizungumzia mchango wa vyombo vya habari kuhusu kutangaza habari za biashara, uchumi na fedha, Dkt. Kessy alisema kuwa Benki Kuu ya Tanzania inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na vyombo hivyo katika maendeleo ya Taifa.

Mada zitakazotolewa ni pamoja na Viwango vya Ubadilishanaji Fedha, Biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, Minada ya Dhamana za Serikali na nyingine nyingi zinazohusu masuala ya Fedha. Semina hii inahusisha washiriki Zaidi ya 43 toka vyombo vya habari vya umma na binafsi na imeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Kwa Zaidi ya miaka minane, Benki Kuu imekuwa ikiendesha semina kwa waandishi wa habari angalau mara moja kwa mwaka ili waweze kuielewa Benki hiyo na kupitia uelewa wao huo waweze kuelimisha umma kuhusu kazi za Benki Kuu na masuala ya Fedha, Biashara na Uchumi kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live