Baada ya Serikali kutangaza kujenga bandari ya uvuvi ya kisasa mkoni Lindi lengo likiwa ni kukuza sekta ya uvuvi na kufanikisha uchumi wa buluu, baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika Wilaya ya Kilwa wameomba elimu juu ya mambo hayo iongezwe katika mitaala
Hayo yameibuka jana Jumanne Septemba 26, 2022 baada ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kutembelea katika shule ya Sekondari ya Kilwa kwa ajili ya kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala ya usafiri kwa njia ya maji.
Aboubakar Khamis, mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule hiyo amesema kuwa wanafunzi wengi wanaomaliza masomo yao wanaishia kukaa mitaani bila ajira kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala hayo na hivyo kusababisha hali ya maisha kuwa ngumu.
"Wananchi wa hapa wengi wanajishughulisha na uvuvi sasa inakuta mtu anachukua mtumbwi anaenda nao hadi katika ya bahari na hapo hana boya na hata kama analo inakuwa haina riflekta hali ambayo inaweza kumsababishiaa majanga.
Kwa upande wake Mwajuma Mohammed ameipongeza TASAC kwa elimu waliyoitoa akidai kuwa yamesaidia kuwafungua akili hasa watoto wa kike ambao walikuwa wanaamini kuwa shughuli za baharini zinafanywa na wanaume pekee.
"Wasichana wengi wanakatishwa tamaa kwa kuambiwa kuwa masomo ya sayansi ni magumu na kwa miaka mingi walikuwa wakilipokea na kuamini kuwa hawawezi lakini kupitia elimu hii tunaamini tutapambana kwa kufuata nyayo za Rais Samia Suluhu Hassan hivyo ninawasihi wasichana wenzangu tuondoe hofu na kuweka juhudi ili baadae tuje kuwa mabaharia na kusimamia taasisi mbalimbali," amesema.
Naye Kaimu Meneja Masoko na Uhusiano wa Umma TASAC, Josephine Bujiku amesema anaamini kuwa elimu waliyoitoa itawasaidia wanafunzi hao na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa juu kuhusu masuala hayo.
"Kupitia mafunzo haya tumelenga kuwaelimisha pia kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya usafirishaji kwa mfano kuna kozi ambazo zina ufadhili wa asilimia 100 yaani mwanafunzi anasoma bure hivyo kwa kuzifahamu itakua rahisi wao kujua ni wapi pa kuanzia," amesema.