Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamiliki wa hoteli za kitalii waombwa kuboresha huduma 

42a0b00948ece1bb72c068ce1572afdb Wamiliki wa hoteli za kitalii waombwa kuboresha huduma 

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imehimiza wawekezaji zaidi katika ujenzi wa hoteli za kitalii na zilizopo, ziboreshe huduma zake kwa gharama nafuu, kila Mtanzania aweze kutalii katika hifadhi mbalimbali za taifa nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alitoa mwito huo juzi wakati akifunga mkutano wa siku nne mjini Morogoro wa wadau wa utalii kwa ajili ya kujadili kuhusu kuongeza idadi ya watalii na mapato, yatokanayo na shughuli za utalii nchini.

Dk Ndumbaro alisema ingawa zipo hoteli za kutosha katika hifadhi mbalimbali nchini , serikali inaendelea kukaribisha uwekezaji zaidi katika sekta ya hoteli kwa ajili ya kutosheleza malazi ya idadi yoyote ya watalii .

"Ukitembelea mbuga za taifa unaweza kulala hoteli ya dola 9,000 kwa siku moja na pia unaweza kulala hoteli kwa shilingi 30,000, huo ni uwezo wa mtu mwenyewe tu ulale wapi , kwa hiyo hoteli zipo nyingi za viwango tofauti ili kuhakikisha kwamba kila mtu anapata stahiki yake,” alisema.

Waziri Ndumbaro alirejelea hotuba ya Rais John Magufuli ya ufunguzi wa Bunge la 12, Novemba 13, 2020 iliyosisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya utalii nchini ili iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Alisema masuala hayo pia yamesisitizwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, hususan katika ibara ya 67.

Alisema kuwa utalii ni sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi, ambayo inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na asilimia 60 ya mapato yote yatokanayo na biashara za huduma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz