Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wamiliki wa hoteli wapata kigugumizi agizo la BoT

Dola Dola Juu Juu Wamiliki wa hoteli wapata kigugumizi agizo la BoT

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kukabiliana na ubadilishaji holela wa fedha za kigeni, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewahimiza wamiliki na waendeshaji wa hoteli za kitalii nchini kuchukua leseni, ili kuanza kutoa huduma hiyo, huku baadhi yao wakilipokea kwa tahadhari.

Tutuba ametoa wito huo wakati wa mkutano na wamiliki pamoja na waendeshaji wa hoteli zinazopokea watalii nchini uliofanyika katika ofisi za Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu, jijini Dar es Salaam jana Machi 14, 2024.

Amewaambia wamiliki wa hoteli 27 waliohudhuria mkutano huo kuwa kwa wao kuwa na leseni itaisaidia Benki Kuu kupata takwimu na taarifa muhimu zitakazosaidia kuimarisha sekta ya fedha.

“Mtakumbuka Oktoba 2023 tulitoa marekebisho ya kanuni ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambapo tulitengeneza dirisha rasmi la kuruhusu hoteli kuanzia nyota tatu hadi tano kuanza kutoa huduma za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni,” amesema Gavana Tutuba.

Akizungumzia msingi wa marekebisho hayo, Gavana Tutuba amesema uamuzi wa kufanya marekebisho ya kanuni hiyo ulitokana na utafiti uliofanywa na kugundua urasimishaji wa maduka ya fedha za kigeni haukugusa hoteli, hivyo kuongeza ubadilishwaji holela wa fedha za kigeni.

“Marekebisho ya kanuni ile yalitokana na utafiti tuliofanya ambapo tuligundua maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokuwa yakiendeshwa yalikuwa bado hayajagusa hoteli, lakini tukakuta hoteli nyingi zinapokea wateja wanaolipa fedha za kigeni, lakini katika fedha zile nyingine zilikuwa zinabadilishwa kiholela.

“Sisi kama wasimamizi wa sekta ya fedha, hatua hii itakuwa fursa ambayo itatufanya tuwe tunapata takwimu za moja kwa moja kwa sababu mtawajibika (hoteli) kuweka ule mfumo wa kupata taarifa ambao utatusaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini,” amesema.

Kwa mujibu wa Tutuba, hadi sasa kati ya hoteli za nyota tatu hadi tano zilizopo nchini, ni Serena pekee ndiyo yenye leseni ya kubadilisha fedha za kigeni.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAP), Edward Kennedy amesema dhamira ya BoT ni nzuri, lakini hadi hoteli kuwa na leseni hizo ni mlolongo mwingine mwingi.

"BoT ingekaa na wadau kwanza, ili kuidadavua hiyo kanuni na kuona itakuwa rahisi kiasi gani kwa pande zote? je BoT itakusanya kiasi gani na mimi mwenye hoteli itamuongezea kiasi gani au itampunguzia kiasi gani?" amehoji Kennedy.

Kuhusu hoteli kuchukua leseni za biashara hiyo, amesema huo ni mchakato ambao utachukua muda hadi wengi wao kufanya, hivyo BoT haina buda kuwakutanisha wadau wote, ili kuwapa uelewa namna ya uendeshaji wa biashara hiyo ya ziada katika shughuli zao.

"Hii ni nia nzuri, lakini biashara ya mwenye hoteli ni malazi na chakula, je akiongeza biashara nyingine ya kifedha, hii kanuni itakuwa na urahisi kiasi gani kuepuka hatari nyingine?" amehoji.

Meneja wa fedha na utawala wa hoteli ya Onomo iliyopo jijini Dar es Salaam, Gosberth Kamugisha, anasema mabadiliko ya kanuni ya kubadilisha fedha za kigeni ni fursa ya ongezeko la mapato kwa hoteli zinazopokea watalii na yataimarisha uchumi wa nchi.

Inaelezwa dola inachangia asilimia 83 ya thamani ya miamala yote inayofanywa kwa ajili ya biashara za kimataifa na sifa kubwa nyingine ni kutumika kama hifadhi ya ukwasu, kwani katika benki kuu zote duniani dola zilizohifadhiwa ni asilimia zaidi ya 60 ya fedha zote za kigeni.

Upatikanaji na mahitaji ya Dola nchini

Kwa takribani mwaka mmoja sasa upatikanaji wa Dola umekuwa ni mgumu katika mataifa mengi tofauti na Marekani, Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yanaendelea kuathiriwa na uhaba wa sarafu hiyo ambayo hutumiwa kwa asilimia zaidi ya 86 katika miamala ya kimataifa, kwa sasa katika masoko rasmi Dola inauzwa kwa Sh2,530 hadi Sh2,600.

Kwa mujibu wa BoT, akiba ya fedha za kigeni hapa nchini ilikuwa Dola bilioni 5.1 hadi kufikia Januari, kiwango ambacho kinatosha kuagiza huduma na bidhaa nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.2 juu ya ukomo uliopo wa miezi minne.

Ripoti ya BoT ya mwenendo wa uchumi ya kila mwezi inaonyesha wastani wa mahitaji yetu ya bidhaa na huduma kutoka nje kwa mwaka thamani yake ni Dola bilioni 16.05, huku mauzo yake ya nje yakiwa Dola bilioni 14.11, hivyo nakisi iliyopo ni Dola bilioni 1.94.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live