Licha ya uongozi wa Manispaa ya Musoma kutumia zaidi ya Sh45 milioni kwa ajili ya kuboresha mazingira na miundombinu ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wamachinga, wamekacha kuyatumia.
Kitendo hicho kinatajwa kuwa ni hasara kwa manispaa hiyo.
Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na vyoo na mabafu na maji.
Maeneo yaliyofanyiwa ujenzi huo wa miundombinu ni Free Park ambalo limebakiwa na wafanyabiashara (machinga) wachache wengi wakiwa wamerudi kandokando ya barabara ya sokoni.
Imeeleza Nyasho na Mlango Mmoja hakuna hata mfanyabiashara mmoja.
Itakumbukwa miaka mitatu iliyopita, Manispaa ya Musoma ilifanya operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo yasiyokuwa rasmi na kuwapeleka katika eneo la Free Park wakaendelee na shughuli zao.
Wakiwa katika eneo hilo, wafanyabiashara hao walilalamikia mazingira mabovu ya kufanya biashara pamoja na eneo hilo kudaiwa kuwa dogo, malalamiko ambayo uongozi wa Manispaa hiyo uliyapokea na kuanza kuyafanyia kazi.
Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Februari 21, 2024 amesema awali alipokea malalamiko kuwa mazingira waliyokuwa wanafanyia biashara hayakuwa rafiki.
"Ni kweli pale Free Park palikuwa padogo na hapakuwa na choo tukatenga si chini ya Sh10 milioni kwa ajili ya ujenzi wa choo na kimekamilika tayari," amesema.
Kuhusu ufinyu wa eneo Gumbo amesema waliamua kutenga eneo lingine la Mlango Mmoja kwa ajili ya wafanyabiashara hao, pamoja na mambo mengine, waliutaka uongozi wa manispaa kujenga barabara pana ya kuingilia sokoni kutokana na ya awali kudaiwa ni finyu.
"Tulibomoa vibada zaidi ya vinne tukatengeneza njia ya kuingia sokoni. Ukumbuke vibanda hivi vilikuwa ni chanzo cha mapato kwa manispaa yetu na lengo letu lilikuwa ni kuwatengenezea mazingira rafiki, tukajenga choo kipya licha ya kuwa kulikuwepo na kingine tukajenga na bafu na kusafisha eneo na kuweka maji hapa tumetumia zaidi ya Sh35 milioni. Lakini hadi sasa hakuna mfanyabiashara hata mmoja aliyeko pale," amesema.
Amefafanua kuwa eneo hilo lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara kati ya 150 hadi 200
Gumbo amesema eneo la Mlango Mmoja lina umbali wa mita 800 kutoka soko kuu na lina uwezo wa kuchukia wafanyabiashara 400 kwa wakati mmoja.
Amesema suala la ukosefu wa wateja na mazingira duni sio sababu tena ya wafanyabiashara hao kushindwa kutumia maeneo yaliyotengwa.
"Mbali na kubomoa vibanda vyetu pale Mlango Mmoja kwa ajili ya kuwatengenezea mazingira kama walivyosema, lakini pia mle ndani kulikuwa na wafanyabiashara wa vibatari, ugoro na vitu vingine ambao wote tuliwahamishia kule eneo la Sido na hawakuwa na pingamizi.
“Lakini cha kushangaza pamoja na jitihada zote hizo bado wamegoma kwenda pale," amesema.
Gumbo amesema baada ya kuona wamachinga hao wameanza kurudi katika maeneo yaliyozuiliwa uongozi wa Manispaa ulichukua hatua kadhaa kudhibiti hali hiyo, hata hivyo hazijazaa matunda.
Amesema hatua hizo ni pamoja na kukamatwa kwa wafanyabiashara sita mwishoni mwa mwaka jana na kufikishwa mahakamani, ambapo walihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini na kila mmoja alilipa faini ya Sh200,000.
"Sisi tumetekeleza wajibu wetu maeneo yaliyotengwa ni rafiki na huduma muhimu zinapatikana suala la kupata wateja linategemea na ubora wa huduma na bidhaa zako mfanyabiashara, hivyo niwaombe wamachinga waende kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa."
Kauli za wafanyabiashara
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko kuu la manispaa hiyo wamesema uwepo wa wamachinga hao kwenye maeneo jirani na soko kunasababisha washindwe kufanya biashara, hivyo wanaiomba mamlaka husika kuingilia kati suala hilo.
"Wanauza vitu ambavyo humu ndani vimo, unafikiri nani atahangaika kuingia humu kununua nyanya wakati ziko hapo nje, Serikali ituangalie maana tunalipa ushuru na kodi zingine," amesema Asha Juma.
Mwenyekiti wa soko hilo, Nyagiro Phinias amesema anashangazwa na kitendo cha wamachinga hao kurejesha biashara zao katika eneo hilo na kusema hali hiyo ni kikwazo cha wao kufanya biashara.
"Kama suala ni kufanya biashara hapa basi waingie sokoni kama sisi maana hadi sasa kuna zaidi ya meza 30 ziko wazi, biashara imekuwa ngumu kwetu sisi hadi watu kufikia kuzifunga."
"Mbali na kulipa ushuru na kodi zote lakini sisi tulioko humu tunategemea biashara hizi kuendesha maisha, wapo watu wana mikopo wanategemea kutoa marejesho humuhumu, sote tuna haki ya kufanya biashara ila tunatakiwa kufuata sheria hawa wenzetu wafuate hawafuati, hatua zichukuliwe ili kutunusuru sisi," ameongeza Nyagiro.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Free Park wamesema hawajui kwa nini wenzao wameamua kurejea katika maeneo ya awali.
"Sio kweli kuwa hakuna biashara hapa, hali ni ngumu kila sehemu lakini kuuza tunauza kinachotakiwa ni uvumilivu tu," amesema Wegesa Manyama muuza samaki.
Wamachinga waliorudi katika eneo hilo lililopo katika barabara ya sokoni wamekataa kuzungumzia jambo hilo huku wakisema hawahitaji waandishi wa habari.
“Hakuna kuongea hapa nyie si huwa mnawasikiliza waliopo sokoni na sisi hatutaki kuongea na nyie, mmeona tumekaa kwa amani hapa mmeamza tena, tokeni bwana."
"Mbona wakati tunapambana ili tuweze kurudi hapa hamkuja kutuhoji leo mmeona tumekuja ndio mnakuja kujisafisha, hatutaki tuacheni tuendelee na mambo yetu," amesema mfanyabiashara mmoja wa nyanya na vitunguu ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kufahamika mara moja.