SHIRIKISHO la Umoja wa Machinga Taifa limelaani vikali uvunjifu wa amani, wizi na uharibifu wa mali za watu wengine ulioripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari kufanywa jana na baadhi ya machinga wa Nyamagana, Mwanza.
“Sisi viongozi wa Taifa wa kundi hili la machinga hatuwezi kufumbia macho kilichofanywa na wenzetu wa Mwanza; sisi siyo wanaharakati wa kuhamasisha fujo, sisi ni taasisi inayoshughulikia mambo kwenye meza ya majadiliano bila kuchoka,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Joseph Mwanakijiji.
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, Mwanakijiji alisema kilichotokea jana ni mwendelezo tu wa matukio ya vurugu za mara kwa mara za machinga katika jiji la Mwanza ambayo yamekuwa yakileta taharuki kwa raia na mali zao.
Akishangaa kwa tukio hilo, alijiuliza kwa nini wanafanya vurugu hizo wakati viongozi wa shirikisho hilo, viongozi wa mkoa na wilaya ya Nyamagana pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum wako kwenye meza ya majadiliano ili kushughulikia changamoto katika masoko ya machinga jijini humo na tayari vikao viwili vimeshafanyika.
Pamoja na majadiliano hayo, Mwanakijiji alisema waliiomba serikali iangalie uwezekano wa machinga hao kuendelea kufanyia biashara zao katikati ya jiji kwa makubaliano maalumu ili kupunguza kilio cha ukosefu wa wateja unaolalamikiwa katika masoko mapya ya machinga.
Alisema uongozi wa shirikisho umepanga kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mwezi huu ili kwa pamoja waweze kuangalia uwezekano wa machinga kuruhusiwa kufanya biashara zao katikati ya jiji muda wa jioni.
“Madai ya machinga yakupelekwa nje ya mji kwa zaidi ya kilometa 14 ambako wateja hawawapati ama hawawafikii ni ya msingi sana lakini yasitumike kuhamasisha uvunjifu wa amani,” alisema.
Aliyataja masoko yanayodaiwa kuwa mbali na kuwanyima wateja machinga hao kuwa ni pamoja na soko la machinga la Igoma Nyamuhongoro na Buhongwe yaliyopo kilometa 15 kutoka katikati ya jiji.
“Haya ni mambo ya kujadiliana na mamlaka sio kufanya vurugu. Tunajua hawa machinga wana mahitaji sawa na binadamu yeyote yule, wanasomesha, wanatakiwa kujenga nyumba, wamepanga nyumba za kuishi na wanalazimika kutunza familia zao, sasa wakipelekwa sehemu ambazo hazifikiki maana yake haki itakua haitendeki,” alisema.
Pamoja na kutoa pole kwa wote walioathiriwa na vurugu hizo, Mwanakijiji aliwaomba machinga wenzake pamoja na viongozi wao huko Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho ufumbuzi wa tatizo hilo unaenda kufanyiwa kazi.