Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliolipwa korosho sasa kutangazwa

47421 PIC+KOROSHO

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Baada ya baadhi ya wakulima wa korosho kulalamika kutolipwa msimu huu, Serikali imesema itabandika majina ya wote walioingiziwa fedha kwenye akaunti zao kila kijiji.

Kutokana na madai hayo kuibua sintofahamu, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema njia ya kumaliza mzizi wa fitina umepatikana na sasa kila kitu kitakuwa bayana.

Hasunga alisema hayo jana alipozungumza na Kamati ya Bunge ya Mifugo na Maji katika ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa. “Sasa naitaka timu ya wataalamu wa operesheni korosho kubandika majina ya wakulima wote waliolipwa kwenye ofisi za kijiji,” aliagiza.

Baada ya mgomo wa wanunuzi wa korosho kwa madai ya bei kubwa tofauti na uhalisia wa soko uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana na kuilazimu Serikali kuzinunua kwa kuitumia bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko, malalamiko ya wakulima hayajaisha.

Waziri Hasunga (pichani) alisema tayari tani 222,684 zimekusanywa hadi Machi 14 na Sh596.9 bilioni zimelipwa kwa wakulima sawa na asilimia 83 ya Sh723 bilioni zinazotakiwa kulipwa.

Alifafanua kuwa hadi Machi 31 wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika.

Wakati inatangaza kununua korosho zote msimu huu, Serikali iliahidi kulipa Sh3,300 kwa kilo ambayo wanunuzi binafsi walishindwa kulipa.

Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, Hasunga aliahidi kuhamia Mtwara kuhakikisha anasimamia vyema mchakato huo mpaka utakapokamilika.

Jana, aliieleza kamati ya Bunge kuwa amegundua mkoa huo unaozalisha karibu nusu ya korosho zote nchini una idadi ndogo ya wafanyabiashara wa korosho kinyume na utaratibu maarufu kama kangomba ukilinganishwa na Lindi yenye wakulima wachache lakini idadi kubwa ya wafanyabiashara hiyo. “Mtwara una wafanyabiashara 10 lakini Lindi wapo zaidi ya 400,” alisema.

Naye mwenyekiti wa kamati hiyo Dk Christine Ishengoma, alimpongeza Hasunga kwa kuanzisha usajili wa wakulima nchini.

“Hakikisha unalisimamia kwa weledi hili ili liwe na matokeo chanya kwani kufanya hivyo Serikali itakuwa na uwezo wa kuwahudumia kwa ufasaha,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz