Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walioibuka kidedea mashindano ya masoko na mitaji kwenda Mauritius

Sat, 27 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanafunzi wanne wa Chuo cha Mipango Dodoma, Chuo Kikuu cha Iringa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Kikuu cha Ardhi wameibuka kidedea katika shindano la masoko ya mitaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini.

Shindano hili lililoandaliwa na Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) lilianza Mei 21, 2018  lililenga kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji ili kuchochea ukuaji wa sekta ya uchumi.

Washindi hao ni Mfaume Ismail wa Chuo cha Mipango wa kwanza katika kundi la washindi wa kujibu maswali kwa upande wa wavulana, Nuru Mkiba kwa upande wa wasichana.

Katika kundi la insha aliyeibuka kidedea ni Winfrida Criment kwa upande wa wasichana  Francis Samba kwa upande wa wavulana ambao wamepata Sh1.8 milioni kila mmoja.

Akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa washindi hao leo Alhamisi Oktoba 25, 2018, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema sekta ya mitaji ni muhimu katika upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni na kusaidia umilikishaji wa umma.

"Pia, itachangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi kwani kadri taifa linavyosonga mbele mahitaji ya fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo hususani miundombinu," amesema.

Dk Mpango ametoa rai kwa mamlaka ya CMSA kuboresha mpango kazi wake wa kutoa elimu kwa umma na huduma zaidi kwa makundi mbalimbali katika kutekeleza jukumu la kuendeleza masoko ya mitaji hasa kwa wananchi walioko vijijini.

"Naomba mashindano haya yawe endelevu na yafanyike kila mwaka ili kuendelea kutoa fursa kwa vijana lakini pia ningeomba lifanyike kwa lugha zote mbili Kiswahili na Kiingereza ili wale wasioelewa Kiingereza wapate nafasi ya kujifunza," amesema.

Waziri huyo amewataka wanafunzi hao kutumia fursa waliyoipata kuelimisha wanafunzi wenzao katika vyuo wanavyosoma ila kuibeba Tanzania katika masuala ya mitaji.

Naye Mwenyekiti wa CMSA, John Mduma amesema katika kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi ya kimataifa ya uwekezaji na dhamana kuendesha mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo yameonyesha chachu kubwa katika kuongeza ujuzi na weledi kwa wahitimu wa mafunzo hayo utakaowezesha kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya maendeleo ya sekta ya masoko ulimwenguni.

Katika mashindano hayo washindi wanne katika nafasi ya pili kwa kundi la kujibu maswali na kuandika isha wamepata Sh1.4 milioni na wengine wanne katika nafasi ya tatu wamepata Sh400,000.

Wahindi hao kumi na mbili wamepata fursa ya kuhudhuria mafunzo nchini Mauritius ambapo watatembelea mamlaka ya usimamizi wa masoko ya mitaji nchini humo.

Akizungumza kwa niaba ya washindi wenzake, Mfaume amesema wanashukuru kwa ushindi huo na wanaamini watakuwa mabalozi wazuri katika kuiwakilisha Tanzania nchini Mauritius.

Chanzo: mwananchi.co.tz