Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walima Tangawizi kunufaika na skimu ya umwagiliaji Mwamba

Tangawizi?fit=1000%2C662 Walima Tangawizi kunufaika na skimu ya umwagiliaji Mwamba

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kilimo cha tangawizi kwa wakazi wa Kata ya Myamba katika Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro kimepata msukumo baada ya Serikali kufanikisha uhakika wa maji kwa ajili ya umwagiliaji.

Uhakika huo unatokana na hatua ya Serikali kutekeleza mradi wa umwagiliaji wa Mwamba-Myamba, ulionufaisha wakulima 4,000 katika eneo hilo na utagharimu Sh1.7 bilioni.

Fedha hizo zilizotolewa zimehusisha ujenzi wa mifereji, uwekaji na ufukiaji mabomba.

Ofisa kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mejason Ayoub, amesema upatikanaji wa maji hayo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa zao la tangawizi, kutoka tani saba kwa ekari za sasa hadi tani 10 kwa ekari baada ya kukamilika kwa mradi.

"Chanzo cha mradi huu ni changamoto iliyokuwepo awali. Maji yalikuwa yanapotea sana na hivyo wakulima wa tangawizi walikuwa wanapata shida katika umwagiliaji,” amesema.

Wakulima wanaonufaika na mradi huo wenye jumla ya ekari za umwagiliaji 2,222.5, kwa mujibu wa Ayoub, ni kutoka vijiji vya Kambeni, Goha na Mang'a.

Kwa mujibu wa Ayoub, shabaha ni kuhakikisha wakulima wa tangawizi katika Vijiji hivyo wanafanya kilimo cha umwagiliaji na hivyo kuongeza tija.

"Matarajio yetu ni kuhakikisha hata wakulima wadogo nao wananufaika na shughuli za kilimo kwa kufanya kilimo cha tija," amesema.

Msifuni Mjema, mkulima wa tangawizi katika kata hiyo, amesema ulifika wakati shughuli za kilimo cha zao hilo kilibaki kuwa shughuli isiyo ya uhakika.

"Kwa sasa tuna matumaini makubwa kwa sababu tumeshaanza kunufaika na mradi wa huu wa skimu ya umwagiliaji," ameeleza.

Mkulima mwingine wa tangawizi katika kata hiyo, Esther Mashika amesema uwepo wa mradi huo umeongeza uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa Februari mwaka jana, unatarajiwa kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta za 1,500 za sasa hadi 2,222.5.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live