Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walalamikia urasimu malipo ya karafuu

F34653cc0711d7be959029cc84132898 Walalamikia urasimu malipo ya karafuu

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) likianza kazi ya ununuzi wa karafuu kwa wakulima Unguja na Pemba, baadhi ya wananchi wamelalamika kuwapo kwa urasimu wa malipo baada ya shirika hilo kuamua kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu na benki.

Mkurugenzi wa ZSTC, Dk Said Seif Mzee alisema juzi kuwa, wameamua kuanzisha utaratibu mpya wa kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu na benki kwa wenye akaunti kwa ajili ya usalama na kuepuka matukio ya uhalifu na uporaji wa fedha.

Alisema matukio ya uhalifu yamekuwa yakiongezeka, hivyo njia salama na muafaka zaidi ni kufanya malipo kwa njia hizo mbili ambazo ni salama kwa wakulima.

Hata hivyo, alisema wapo tayari kusikiliza changamoto na ushauri zaidi ambao utafanikisha malipo kwa wakulima wanaouza karafuu zao katika vituo vya karafuu vilivyopo Unguja na Pemba.

Baadhi ya wakulima waliofika katika vituo vya kuuza karafuu Unguja wametoa malalamiko yao ya kuwapo kwa urasimu na vikwazo vingi vyenye kukatisha tamaa.

Lailati Hussein (21) aliyefika katika kituo cha kununua karafuu Saateni mjini Unguja akiwa na kilo sita za zao hilo, alisema amepata usumbufu mkubwa na kulazimika kurudi na karafuu zake nyumbani baada ya kutakiwa kuonesha vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi pamoja na barua kutoka kwa sheha na jina la mmiliki wa shamba alilochuma karafuu.

“Maswali yalikuwa mengi kwa hiyo nimelazimika kurudi nyumbani nikiwa na karafuu zangu kwa sababu, kwanza sikuwa na jina la shamba nililochuma karafuu zaidi kwa sisi wanafunzi huwa tunaokota karafuu zilizoanguka chini maarufu kwa jina la mpeta,” alisema.

Mkulima anayemiliki shamba maeneo ya Kitumba, wilaya ya Kati Unguja aliyejitambulisha kwa jina la Salum Sadi ambaye alifikisha karafuu zake magunia mawili, aliambiwa kwanza anahitaji kupata barua kutoka kwa sheha wake, huku akilazimika kuonesha waraka wa eka anayoimiliki.

“Haya ni masharti mapya hatukuyazoea katika kipindi cha miaka ya nyuma, mimi kwa zaidi ya miaka 30 hivi sasa nauza karafuu zangu ZSTC,” alisema.

Wakulima wengine ambao wameanza kuuza karafuu zao na kulipwa kwa njia ya miamala ya simu wamelalamika makato makubwa yanayofanywa wakati wa kupokea fedha zao kwa mawakala.

“Niliuza karafuu zangu na kulipwa fedha wastani Sh 300,000, lakini fedha zilizokatwa zilikuwa nyingi Sh 10,000 katika muamala wa simu wakati wa kutoa,” alisema.

ZSTC imeanza kununua karafuu kwa wakulima katika msimu mdogo wa mavuno na kuanzisha utaratibu mpya wa kulipa fedha kwa wakulima kwa njia ya miamala ya simu au akaunti za benki.

Chanzo: www.habarileo.co.tz