Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walalamikia tozo ya madumu matupu kwa Waziri Bashungwa

Bashungwa: Rais Samia Yupo 'serious' Na Ujenzi Wa Barabara.jpeg Walalamikia tozo ya madumu matupu kwa Waziri Bashungwa

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameuagiza uongozi wa Serikali Wilaya ya Musoma kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kutatua kero ya wananchi kulipishwa gharama ya kusafirisha madumu matupo katika kivuko kinachosafirisha abiria na mizigo kati ya Mwigobero- Kinesi.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 10, 2023 baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi, hasa wajasiriamali kutoka Kinesi wanaosafisha madumu ya maziwa kutoka Kinesi kwenda Musoma mjini.

Amri hiyo imetokana na mmoja wa wajasiriamali, Elizabeth Innocent, mkazi wa Kinesi Wilaya ya Rorya kumweleza Waziri Bashungwa kuwa wanatozwa gharama ya Sh500 wanaposafirisha dumu la lita 20 lenye maziwa wakati wa kwenda mjini Musima na Sh200 kwa dumu tupu wanaporejea nyumbani.

"Hatuna tatizo kulipia Sh500 kusafirisha madumu yenye maziwa wakati tunaenda kufanya biashara mjini Musoma; lakini siyo haki kutozwa tena gharama ya Sh200 kwa kila madumu matupu tunaprejea nyumbani,’’ amesema Elizabeth

Akizungumzia kero hiyo, Waziri Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa lengo la Serikali kununua vivuko ni kutoa huduma na siyo biashara, hivyo uchangiaji wa gharama lazima uwe rafiki na ulenge kutoa huduma.

"Serikali haijaleta kivuko hiki kwa ajili ya kufanya biashara na kupata faida; lengo ni kutoa huduma kwa wananchi. Naagiza viongozi wa Serikali Wilaya za Musoma na Rorya kwa kushirikiana na Temesa kukaa chini kutatua kero hii inayolalamikiwa na wananchi,’’ amesema na kuagiza Waziri Bashungwa

Amesema badala ya kufikiria na kuweka mbele tozo zinazochangia hali ngumu ya kiuchumi kwa wananchi, ni vema wahisika watafute namna ya kuongeza ustawi kiuchumi kwa wananchi, jambo ambalo ndilo lengo na jukumu la Serikali.

Kuhusu kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika mwalo wa Mwigobero, Waziri huyo ameupa uongozi wa Temesa hadi Desemba 25, mwaka huu kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kuwaondolea abiria adha ya kunyeshewa mvua nyakati za masika na kuchomwa jua wakati wa kiangazi wanaposubiri kivuko.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi a jengo la abiria katika mwalo huo kwa gharama ya zaidi ya Sh283 milioni ulianza tangu Agosti, 2021 lakini haujakamilika hadi sasa.

Mbunifu wa Majengo kutoka Ofisi ya Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Mara, Celestine Kaitaba amemweleza Waziri kuwa mradi huo unatekeleza na Kampuni ya Corporation Sole na umefikia asilima 35 ya utekelezaji.

‘’Ukikamilika, jengo hilo litakalokuwa na huduma zote muhimu itahudumia abiria 225 waliokaa kwa wakati mmoja,’’ amesema Kaitaba

Diwani wa Kata ya Mwigobero, Mariam Sospeter (CCM) ameiomba Serikali kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati kuwaondelea wananchi kero ya kupigwa jua na kunyeshewa wanaposubiri kivuko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live