Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walalamikia lumbesa biashara ya viazi mviringo

Lumbesa Walalamikia lumbesa biashara ya viazi mviringo

Tue, 20 Jul 2021 Chanzo: ippmedia.com

Wakulima hao wamekiita kitendo hicho kwamba ni unyonyaji dhidi yao.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali Kuu kuingilia kati kudhibiti ujazo huo kwa maelezo kuwa halmashauri yao imeshindwa kutatua kuwafanya waendelee kunyonywa na kuwafanya waendelee kuwa maskini.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Isapulano, walisema wamekuwa wakishindwa kuwakatalia wanunuzi kuendelea na mfumo huo kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

Felister Salat, alisema wanunuzi hao wamekuwa wakiwatishia kwamba wasipokubaliana na ujazo huo viazi vyao havitanunuliwa, hali ambayo huwalazimisha kukubali kuuza, huku wakijua wanaumia.

“Wanunuzi wanakwambia hawatanunua viazi vyetu bila kujaza lumbesa, sasa unajikuta watoto wanatakiwa kula, kusoma na matumizi mengine muhimu, kwa hiyo tunakubali hivyo hivyo, japo tunaumia sana,” alisema Felister.

Naye Heneriko Sanga, alisema wakati wa kulima hakuna mtu anayewasaidia gharama za uzalishaji kwa maelezo kuwa hata kama pembejeo zinauzwa kwa bei ghali hupambana wenyewe, lakini tatizo linaanza baada ya kuvuna.

Alisema wananunua mbolea ambayo ujazo ni ule ule nchi nzima, lakini wanunuzi wa viazi wanataka kununua viazi vyao kwa ujazo wa lumbesa, lakini hakuna ofisa yeyote wa serikali wilayani humo ambaye amekuwa akiwasaidia.

Baadhi ya wanunuzi wa viazi walisema wanaendelea kutumia lumbesa kutokana na biashara ya viazi kuwa ngumu sokoni, hivyo wanatumia ujazo huo kama sehemu ya kuwavutia wateja wanunue haraka kwa maelezo kuwa zao hilo likikaa muda mrefu linaoza.

Mmoja wa wanunuzi hao, Abbas Omary, alisema mbali na kuvutia wateja pia Halmashauri ya Makete imegeuza utaratibu huo kuwa kitega uchumi kwa kuwatoza ushuru maalum kwa ajili ya ujazo huo.

“Tunatoa ushuru wa kawaida wa ununuzi wa mazao, lakini tunatozwa Sh. 1000 kama faini ya lumbesa, sasa hatuoni sababu ya kuacha kuutumia utaratibu huu,” alisema Omary.

Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Makete, Sylivester Mbawala, alikiri kuwa lumbesa imeshapigwa marufuku, ingawa bado inaendelea kutokana na wakulima kuonekana wanaridhika na utaratibu, na kwamba wao wana jukumu la kuwasaidia wazalishe kwa tija.

Alisema endapo wakulima watashirikiana na serikali, kuna uwezekano utaratibu huo ukafika kikomo lakini kwa kuwa wanaridhika ni vigumu kuukomesha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Francis Namaumbo, alikiri kuwatoza tozo za ziada wanunuzi wanaonunua viazi kwa lumbesa, kwa maelezo kuwa lengo sio kuchochea biashara hiyo bali ni sehemu ya mikakati ya kuukomesha.

Alisema fedha hizo zikishakusanywa halmashauri inazirudisha kwa wakulima kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Chanzo: ippmedia.com