Geita. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wamewataka wakulima wa pamba kutokubali kuuza zao hicho chini ya bei elekezi ya Sh1,200.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 21, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato (CCU) pamoja na wananchi kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato kinachomilikiwa na CCU.
Amesema wakulima waendelee kuwa na subira kwa sababu wanunuzi hao wamepewa fedha za kutosha kununua pamba yote kwa bei hiyo, si vinginevyo.
“Hata mkiwa na shida msikubali kuuza pamba yenu chini ya Sh1,200 kwa kuwa haitachukua muda mrefu mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa kuna wanunuzi wamepata fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai wakulima kwa kutaka kununua kwa Sh800, msikubali na mkiwaona mtupe taarifa,” amesema Majaliwa.
Amesema viwanda vya nyuzi na nguo vikijengwa nchini kutakuwa na uhakika wa soko kwani hivi sasa Tanzania haina viwanda vya kutosha vya nguo.
Amebainisha kuwa Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania na mwekezaji atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina hiyo kwa sababu mahitaji ni makubwa.
Pia Soma
- kusuasua usajili laini za simu kwazua jambo, Majaliwa aionya Nida
- Alikiba arudi Shule ya Msingi Upanga
- Diamond awa kivutio maonesho ya utalii Iringa
Awali, meneja wa CCU, Charles Nyasi alimueleza Majaliwa kuwa kampuni ya METEL, KCCL na FRESHO zimejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari kilo 9,611,860 zimenunuliwa kati ya kilo 11, 140,529 zilizokusanywa.
Amesema kampuni ya FRESHO imenunua kilo 4, 869, 960; KCCL kilo 3, 025,051 na METEL kilo 1,716, 420.
Ameiomba Serikali isaidie kuwalipia deni la Sh696 milioni ili kumaliza tatizo la madai ya watumishi na wadai wengine, “Pia Serikali isaidie kuilipia CCU deni la Sh102 milioni la ardhi waliyotumia kujengwa kiwanda chao.”
Akijibu maombi hayo, Majaliwa amesema Serikali haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa maelezo ya kina ni nani aliyelisababisha.