Baadhi ya wakulima mkoani Kigoma wameiomba serikali kurudisha mfumo wa zamani wa upatikanaji wa mbolea kwa madai kwamba mfumo uliopo umekuwa na changamoto ikiwa ni pamoja na kutumia muda mrefu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakullima hao kutoka wilaya ya Uvinza na manispaa ya Kigoma Ujiji wamesema mfumo huo unatumia muda mrefu wao kupata mbolea hizo hali inayoweza kusababisha hasara katika mazao yao.
Mkulima kutoka wilaya ya Uvinza, Modesta Sokomo amesema kwasasa anahitaji mbolea ya kukuzia mazao yake na ameshafanya taratibu zote ikiwemo kujiandikisha lakini amepangiwa tarehe ya mbali ambapo mazao yake yapo hatarini kuharibika kwa kukosa mbolea.
“Serikali iangalie upya huu utaratibu wa kupata mbolea ya ruzuku, umekuwa na usumbufu mkubwa na unatumia gharama kubwa kufatilia mbolea kuliko mbolea unayotaka lakini pia muda unakuwa mrefu wa kufuatilia mbolea huku mazao yanaendelea kukua na mvua zinanyesha,” amesema Sokomo.
Kwa upande wake, mkulima kutoka Mkongoro halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Ramadhani Shauri amesema amefika katika eneo hilo kufata mbolea ikiwa ni siku tatu mfululizo bila mafanikio na wakati mwingine wanaambiwa mtandao unasumbua.
“Mfumo uliopo unakatisha tamaa, makulima hasa sisi wadogo wadogo kipato chetu ni kidogo kila siku kutumia nauli kuja mjini kufuatilia mbolea na hatuipati kwa wakati, ni bora serikali ikatazama upya mfumo huu na kuturudishia mfumo wa awali ambao hauna usumbufu,” amesema Shauri.
Mwakilishi wa kampuni ya usambazaji wa mbolea ya ruzuku ya Export Trading Group (ETG), Donald Balton amesema upatikanaji wa mbolea katika kampuni yake unaridhisha isipokuwa baadhi ya mbolea zimewaishia ambazo ni mbolea aina ya CAN na UREA zote za kilo 50 na utaratibu wa kuzipata unaendelea.
Amesema kwa siku moja wanaweza kuhudumia wakulima 100 hadi 150 kama mtandao utakuwa vizuri kwani moja ya changamoto za kuwepo kwa msongamano ni pamoja na kusuasua kwa mtandao wakati mwingine na kushindwa kufikia hata watu 50 kwa siku.
Ofisa kilimo mkoa wa Kigoma, James Peter amesema ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa mawakala wa mbolea waliosajiliwa na mamkala ya mbolea nchini ni miongoni mwa sababu zilizosababisha changamoto ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakati.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo ya ukosefu wa mbolea ya ruzuku kwa wakati kwa wakulima, serikali imeagiza kila halmashauri kuhakikisha wanawasilisha maeneo ambayo wanadhani ikipelekwa mbolea itapunguza adha na usumbufu wanaopata wakulima hasa maeneo ya vijijini.
Kwa mkoa wa Kigoma kuna kampuni mbili zinatoa huduma ya mbolea ya ruzuku ambapo katika wilaya ya Kasulu na Kibondo wana matawi na kutoa huduma kwa wakulima katika maeneo hayo.