Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wataka bei ya pembejeo ishushwe

50964 Pic+kasulu

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kasulu. Wakulima wadogo mkoani Kigoma wameiomba Serikali kushusha bei ya mbolea ya kupandia na kukuzia kwa takribani asilimia 50.

Wakulima hao wametaka bei kushuka kutoka Sh70,000 kwa kilo 50 hadi Sh40,000 kwa mbolea ya kupandia na Sh40, 000 hadi Sh20,000 kwa mbolea ya kukuzia.

Hayo yalibainishwa jana Jumamosi Aprili 6, 2019 wakati wa mafunzo ya matumizi bora ya mbolea kwa wakulima na mawakala wa pembejeo yaliyotolewa na Kampuni ya GS Agro.

Mkulima Saidi Shaban alisema ni bora mkulima akawekewa ruzuku kwenye mbolea kwani bei ikiwa chini hata mkulima wa hali ya chini ataweza kumudu gharama za kununua mbolea na kulima kilimo cha kisasa.

"Wenyeji wa wilaya hii tunatumia pembejeo zetu kwa mazao ya chakula na biashara ambayo ni mahindi na maharage sasa tunaposhindwa kuyahudumia vizuri mazao hayo tunakosa vitu viwili kwa wakati mmoja," alisema Shaban.

Mwezeshaji wa wakulima kutoka kijiji cha Msambala Fatuma Bahi, amesema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni upungufu wa maofisa ugani na kupelekea kata zaidi ya tatu kuhudumiwa na mtu mmoja.

Amesema wakulima wameshindwa kufikia malengo yao kwa kukosa elimu kutoka kwa maofisa ugani kwani wamekuwa wakihudumia watu wengi huku wengine kukosa nafasi ya kuonana naye.

"Serikali ikitaka kuboresha kilimo lazima pia waongeze maofisa ugani katika kata na vijiji ili kuwafikia wakulima wengi kwa wakati huku wakitoa bei nzuri za pembejeo ili kila mkulima aweze kumudu," alisema Bahi.

Mhandisi kilimo na umwagiliaji mkoani hapa, Yohana Zephania amesema wakulima wengi hawatumii pembejeo za kilimo badala yake hufanya kilimo cha mazoea lakini kama watatumia vizuri mbolea watakuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Mkuu wa mauzo kutoka kampuni ya GS Agro, Remi Nindi, alisema mbali na kuuza mbolea kwa wakulima pia wamekuwa wakiwatembelea wakulima wao mara kwa mara na kuwaelimisha na kujua changamoto zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz