Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima watahadharishwa na matapeli

SOKO LA KIBAIGWA.webp Wakulima watahadharishwa na matapeli

Thu, 30 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKULIMA wameshauriwa kutumia soko la kimafaifa la mazao Kibaigwa wilayani Kongwa, kuuza mazao yao ili kuepuka kutapeliwa na walaguzi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kongwa, Dk. Omari Mkulo, wakati alipozungumza na Nipashe jana ofisini kwake kuhusu mikakati ya ukusanyaji wa mapato katika soko hilo la kimataifa la mazao.

Dk. Mkulo aliwashauri wakulima kutumia soko hilo kuuza na kununua mazao ili kuepuka kuingia mikononi mwa walanguzi wa mazao wasio waaminifu.

“Ninawasihi ndugu zangu wakulima wa Kanda ya Kati na mikoa ya jirani na Kibaigwa kutumia soko letu la mazao Kibaigwa kwa sababu watakuwa na ukakika kupima mazao yao kabla ya kuuza tofauti na mitaani watatapeliwa,” alisema.

Alisema msimu wa mavuno ya mazao umeshaanza na kuna baadhi ya walaguzi wameshaanza kuwafuata wakulima mashambani wakiwalaghai kununua kwa makadirio bila kutumia mizani.

Pia, alisema mkulima kutumia madebe au kukadiria ya gunia yatawasababishia hasara kwa sababu hakuna ukakika wa uzito wa mazao anayotarajia kuuza kwa mfanyabiashara.

Alitaja mikakati waliyonayo katika kuhakikisha wanadhibiti upotevu wa mazao kuwa wamebadilisha muundo wa uongozi wa soko kwa kuweka watumishi waajiriwa wa halmashauri.

Aliwataja viongozi wapya waliowekwa kuwa ni meneja na katibu wa soko hilo watakaokuwa na wajibu wa kusimamia mapato yote yanayoingia hapo kila siku na kusimamia shughuli zote.

Pia alibainisha kuwa halmashauri hiyo imekuwa ikikusanya zaidi ya Sh. milioni 511 kwa mwaka kutokana na mapato ya soko hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa soko hilo, Imani Matonya, alisema msimu wa mazao umeanza na soko limeanza kupokea mazao kila siku na kuuza.

Matonya alisema kwa sasa wanatoa tani zaidi ya 10,000 ya mazao ya mahindi kwa siku na mategemeo ni kuongezeka mizigo zaidi kwa siku zijazo.

Alisema mahindi wanayopokea kwa sasa yanatoka mikoa ya Dodoma, Morogoro hasa Wilaya ya Gairo na Mkoa wa Tanga, wilaya ya Kilindi na Handeni.

Alibainisha kuwa bado hawajaanza kupokea mazao kutoka Mkoa wa Manyara kutokana na mvua kuendelea kunyesha eneo hilo.

Alisema makusanyo ya ushuru wa mazao sokoni hapo ni wastani wa Shilingi milioni mbili hadi tatu kwa siku na mahindi yananunuliwa kwa Sh. 500 hadi 550 kwa kilo katika kipindi hiki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live