Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima washauriwa kutumia teknolojia

Kilomo Teknolojia Wakulima washauriwa kutumia teknolojia

Thu, 3 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKULIMA wametakiwa kuchangamkia teknolojia ya kisasa ya kutumia ndege nyuki (drone), katika upulizaji wa dawa katika mashamba yao, upandaji wa mbegu, kuangalia usalama wa shamba kwa kuchukua picha na kuweka ramani kwa ajili ya mipango mingine.

Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Yessaya Mwakifulefule amesema hayo katika maonesho ya nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

“Hii ni teknolojia mpya imekuwa kwa kasi sana. Mashamba makubwa kama Mtibwa wanatumia teknolojia hii, pia mashamba ya Mbarali wanatumia,” amesema.

Amesema katika msimu huu wa nanenane wapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu teknolojia hiyo na kuelekeza wapi inapatikana.

Pia amesema wanatoa elimu kwa ajili ya anga la chini ambapo ndege nyuki ndipo zinaporuka.

“Tunatoa elimu kwa ajili ya anga la chini ambalo lilikuwa halitumiki vizuri kwa muda mrefu sana. Kwa kuwa sasa drones zinatumika kwenye kilimo na kuna wakulima wengi sana nchini wana eka 10 ama 20 hizo sio mchezo kuzipuliza dawa kwa njia ya kawaida lakini teknolojia hiyo inarahisisha.

“Sasa tukitoa elimu hii kwa wakulima wakahamasika na kununua drones na wakalipia vibali, wao watanufaika na shughuli zao za kilimo zitarahisishwa na sisi mamlaka tutanufaika tutakuwa tumeingiza fedha. Kama mamlaka ni wajibu wetu wa kubadilisha matumizi ya teknolojia katika kilimo,” amesema.

Amesema mpaka sasa kuna ndege nyuki 15 zinazotumika katika kilimo hapa nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live